KINSHASA: Ujerumani itaendelea kuisadia Kongo
27 Septemba 2006Matangazo
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani,Franz Josef Jung amesema,Ujerumani itatoa msaada wa muda mrefu kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Baada ya kukutana na makamu wa rais,Jean Pierre Bemba mjini Kinshasa,waziri Jung alisema,serikali ya Ujerumani haitositisha msaada wake,hata baada ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Ulaya EUFOR kuondoka Kongo mwishoni mwa mwezi wa Novemba. Wakati huo huo amesema,muda wa vikosi vya Ujerumani kubakia nchini Kongo hautorefushwa. Akaongezea kuwa anaamini duru ya pili ya uchaguzi wa rais mwezi wa Oktoba utakwenda kwa amani. Katika uchaguzi huo,Bemba atapambana na rais wa sasa Joseph Kabila,ambae bila ya kutoa sababu, muda mfupi kabla ya kukutana na Jung alifuta mkutano huo uliopangwa tangu hapo awali.