KINSHASA : Polisi hawakuamuriwa kutumia risasi za moto
3 Julai 2005Mwanasiasa mwandamizi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo amesema hapo jana kwamba polisi waliokuwa wamepewa majukumu ya kusimamia maandamano mapema wiki hii hawakupewa amri ya kutumia risasi za moto.
Viongozi wa upinzani wamedai kwamba takriban watu 26 wameuwawa hapo Alhamisi wakati polisi ilipovunja maadamano kwenye miji kadhaa juu ya kwamba serikali imesema ni watu 10 tu waliouwawa wakati polisi ilipopambana na waandamanaji.
Azarias Ruberwa mmojawapo wa makamo wa rais wanne nchini Congo amewaambia waandishi wa habari kwamba polisi waliagizwa kutotumia risasi za kweli na kwamba uchunguzi unafanyika kujuwa wahusika.
Maandamano hayo yaliitishwa kupinga kushindwa kufanya uchaguzi kama ilivyopangwa awali kwa kuzingatia mkataba uliotiwa saini na serikali na makundi ya waasi hapo mwaka 2003 ambao umekomesha vita vya miaka mitano vilivyozusha maafa makubwa.