Kimbunga Kajiki chapiga kusini mwa China kikielekea Vietnam
25 Agosti 2025Matangazo
Kiasi ya watu 20,000 walihamishwa kutoka maeneo yanayoweza kuwa hatari kabla ya dhoruba hiyo. Boti za wavuvi zilirejea bandarini na zaidi ya wafanyakazi 21,000 wakahamia maeneo salama.
Kimbunga Kajiki kilitarajiwa kutua kwenye pwani ya Vietnam Jumatatu mchana. Maafisa nchini humo walikuwa wanajiandaa kuwahamisha zaidi ya watu 500,000 kutoka majimbo manne ya pwani ya kati. Zaidi ya kaya 150,000 katika mikoa ya Thanh Hoa, Quang Tri, Hue na Danang waliamrishwa kutafuta hifadhi mbali na maeneo ya pwani. Mashirika ya ndege ya Vietnam yalifuta safari kutokana na hali mbaya ya hewa iliyotarajiwa. Wataalamu wa hali ya hewa wanasema Kimbunga Kajiki kinavuma kwa kasi ya kilomita 175 kwa saa. Mvua kubwa na mafuriko vinatarajiwa.