Kima cha chini cha mishahara Ujerumani chaongezwa
27 Juni 2025Kulingana na tume inayohusika na kima cha chini cha mishahara, kiwango hicho kitaongezeka kutoka yuro 12.82 kwa saa hadi yuro 14.60 ifikapo 2027.
"Ni vyema tume ya kima cha chini cha mishahara ikafikia muafaka," Katibu Mkuu wa CDU Carsten Linnemann aliiambia DPA baada ya uamuzi huo uliotangazwa siku ya Ijumaa.
"Huu ni ushirikiano wa kijamii kwa vitendo na inaonyesha kuwa tume inafanya kazi. Kupanga mishahara litabaki kuwa suala litakalowahusisha washirika kwenye mazungumzo kama hayo katika siku zijazo."
Linnemann ambaye chama chake kimo ndani ya serikali ya mseto inayojumuisha chama ndugu cha Bavaria cha Christian Social Union - CSU - walikuwa wametoa wito wa kima cha chini cha mshahara kuongezwa hadi yuro 15.
Tume ya Kima cha chini cha Mshahara, inayoundwa na wawakilishi wakuu wa vyama vya wafanyakazi na waajiri pamoja na rais huru, hupiga kura ya marekebisho ya mishahara kila baada ya miaka miwili, kwa kuzingatia ukuaji wa vipato.
Kima cha chini cha mshahara wa sasa kinacholipwa kisheria kwa wafanyakazi ni yuro 12.82.
Katika hatua nyingine, Bunge la Ujerumani limepiga kura ya kuzuia familia za wakimbizi kuungana bila ya kuwa na hadhi ya kudumu ya muomba hifadhi, hatua ambayo ni sehemu ya mpango wa Kansela Friedrich Merz ya kuimarisha sheria za uhamiaji.
Sheria hiyo mpya, iliyopitishwa Ijumaa na Bunge-Bundestag, inamaanisha kwamba watu ambao hawana hadhi ya ukimbizi lakini wanaishi Ujerumani kutokana na kitisho kikubwa kwa maisha yao katika mataifa waliyotoka, hawataweza kuwaleta watu wa karibu nchini Ujerumanikatika kipindi cha miaka miwili ijayo.