Kim Jong Un asafiri Beijing kuhudhuria gwaride la kijeshi
2 Septemba 2025Kim Jong Un anatarajiwa kuungana na Rais wa China Xi Jinping, Rais wa Urusi Vladimir Putin na viongozi wengine wa dunia katika tukio hilo la kihistoria ambapo China itaonesha nguvu zake za kijeshi.
Gwaride hilo litahusisha wanajeshi kupita kwa mpangilio maalum, ndege za kivita kuruka angani, pamoja na vifaa vya kisasa vya kijeshi vinavyoakisi uwezo wa taifa hilo kijeshi na kiteknolojia.
Zaidi ya viongozi 25 wa dunia wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo itakayofanyika katika Uwanja wa Tiananmen, jijini Beijing, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
China imekuwa ikitangaza gwaride hilo kama ishara ya mshikamano wa kimataifa, na ushiriki wa Kim Jong Un unatarajiwa kuwa wa kihistoria, kwani hii itakuwa mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa Korea Kaskazini kuonekana hadharani pamoja na Xi na Putin katika hafla moja.