Kilichoandikwa leo na Magazeti ya Ujerumani
21 Machi 2005Kwanza tuanze na siasa za ndani za hapa Ujerumani, na tuelekee Kiel, mji mkuu wa Mkoa wa Schleswig Holstein. Gazeti la BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG liliichambua hali hiyo kama hivi:
Kwa serekali ya mseto ya shirikisho ya vyama vya Social Democratic, SPD, na Kijani, mkoa wa North Rhein Westfalia sasa ndio ngome ya mwisho ya kuitetea kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Shirikisho Oktoba mwakani. Pindi vyama hivyo vitashindwa katika uchaguzi wa Mkoa wa North Rhein Westfalia hapo Mei mwaka huu, basi kutarajiwe kuweko mabadiliko katika serekali ya shirikisho mjini Berlin. Nini kitakachokuja baadae? Serekali ya mseto ya vyama vikuu inaweza kuwa ni ushiriki wa dharura ili kurejesha imani ya wananchi kwa serekali na kwa pamoja kuleta marekebisho yanayohitajiwa. Serekali hiyo itakuwa ya muda fulani, tena ilioungana kupambana na mbinyo na upinzani wa kutoka jumuiya za wafanya biashara na matajiri, vyama vya wafanya kazi, jumuiya za kutetea maslahi ya kijamii na pia jumuiya yenye kuwatetea walipaji kodi. Pindi hayo yatafanyika, basi nchi itaweza kusonga mbele vizuri. Huenda, lakini, mambo yakawa kinyume na hivyo.
Gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE linalochapishwa mjini Erfurt liliuliza kama sererekali ya mseto ya vyama vikuu vya SPD na CDU itakuwa ni mfano mzuri kwa Ujerumani? Gazeti hilo linahisi fikra hiyo inatiwa chumvi sana. Hata hivyo, mjadala huo wote utabidi uishie angalu mwezi wa Mei pale wapigaji kura watakapochagua serekali ya Mkoa wa North Rhein Westfalia. Kuna wiki chache hadi wakati huo, lakini ishara zinaonesha sana kwamba Chama cha Social Democratic, SPD, kitashindwa katika eneo lake la kisiasa la asili na serekali ya mkoa huo kuchukuliwa na Chama cha Christian Democratic, CDU. Hapo tena njia itakuwa wazi kwa Bibi Angela Merkel kuwa kansela wa shirikisho.
Vivyo hivyo ndivyo linavoona gazeti la Rhein-Neckar-Zeitung la kutokea Heidelberg. Linahoji kwamba pindi Kansela Gerhard Schroader hatovunjika moyo, na waziri wa mambo ya kigeni, Joschka Fischer, hatoshindwa katika mkasa unaohusu ubalozi wa Ujerumani wa Kiev kutoa Viza za kinyemele kwa Wa-Ukraine kuja hapa Ujerumani, basi haitokuwa hata kidogo kwa maslahi ya Chama cha CDU kutaka kuwa na serekali ya mseto ya vyama vikuu. Ikiwa sasa ina wingi katika Baraza la serekali za mikoa, Bundesrat, na wingi huo utazidi pindi kutakuweko mabadiliko ya serekali katika Mkoa wa North Rheine Westfalia, basi chama hicho cha CDU pindi kitashinda katika uchaguzi mkuu wa mwakani kitaweza kutekeleza mkakati wake wa kuleta marekebisho, tena bila ya kizuwizi chochote.
Kuhusu hali ya mambo katika serekali ya mseto ya shirikisho ya vyama vya SPD na Kijani ya mjini Berlin, gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG limeandika kwamba kiongozi wa chama tawala cha SPD, Franz Müntefering, mtu ambaye hapendi malumbano, yaonesha sasa amevaa njuga na kukishambulia chama kidogo shirika serekalini, yaani Chama cha Kijani. Takwa la kiongozi huyo kukitaka chama cha Kijani kioneshe utahbiti zaidi ni alama ya kuvunjika moyo chama cha cha SPD cha Franz Münterfering. Kwamba Chama hicho cha kijani kimeweza kupata nyongeza ya asilimia mia moja ya kura ya maoni ya watu, licha ya kuwa pia na dhamana ya kuregea uchumi wa Ujerumani, kushindwa kupata mafanikio kutokana na mpango wa kukuza nafasi za kazi uliopewa jina la Hartz Nambari nne na mkasa wa kutolewa Viza kinyemele katika ubalozi wa Ujerumani mjini Kiev ni jambo linalokifanya chama cha SPD kizidi kuwa na uchungu.
SÜDDEUTSCHE ZEITUNG la mjini Munich lilisema kwamba katika serekali ya mseto inayoongozwa na Gerhard Schroader na Joschka Fischer matamshi yamekuwa makali zaidi, na makali hayo yanatokana na mkasa wa siasa iliokuwa inafuatwa ya kutoa Viza katika Ubalozi wa Kiev, kutokana na mabishano kuhusu mswada wa sheria ya kuondosha ubaguzi -hayo yote ni mambo yalio katika nyoyo za wanachama wa SPD kwani yamehatarisha nafasi za kazi. Na mambo yamezidi kuwa mabaya baada ya kushindwa waziri kiongozi wa Schleswig Holstein, Bibi Heidi Simonis, kuchaguliwa tena. Lakini hayo yote hayana umuhimu mkubwa na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwakani. Hisia za kisiasa hapa nchini zinabadilika hivi sasa tukiingia katikati ya mwaka. Mnamo muda mfupi mambo yote yanaweza yakabadilika, kuelekea njia nyingine.
Gazeti la TAGESPIEGEL la mjini Berlin halina matumaini makubwa juu ya kutekelezwa ule uamuzi uliofikiwa katika mkutano wa kilele baina ya serekali na upinzani kuhusu kutafuta njia za kuunda nafasi za kazi. Linaona kwamba baada ya mkutano huo uliozungumziwa sana kwa mbwembwe, wale waliopanda kilele sasa wamerejea katika kambi zao. Nini kile ambacho kitafuata ni kila upande kuulaumu upande mwengine juu ya namna mapendekezio hayo yatakavoweza kugharimiwa.Gazeti hilo lilidai kwamba kwa wanasiasa hao mbinu za kisiasa kwa wao ni muhimu zaidi kuliko kuweko maendeleo ya kisiasa. Kila upande unahisi mafanikio yanaweza kuwa ya hatari pindi yatadaiwa na upande wa pili.
Mwishowe tuliangalie gazeti la WESTDEUTSCHE ALLGEMEINE ZEITUNG ambalo liliandika juu ya mipango ya kuufanyia marekebisho Umoja wa Mataifa. Liliandika hivi:
+Ingekuwa Umoja wa Mataifa hauko, basi mtu ingebidi auvumbuwe. Kwa upande mwengine, huu Umoja wa Mataifa tulio nao usingekuwa na haki ya kudai kile unachofanya sasa. Kwa hivyo, ni wakati sasa kwa Umoja wa Mataifa kuvumbuliwa upya. Katibu mkuu wa Umoja huo, Kofi Annan, hivi sasa anafanya jaribio jipya, huenda jaribio la mwisho linalowezekana, kuufanya Umoja wa Mataifa mwishowe uwe kama vile walivotaka waasisi wake. Ripoti ya kurasa 63 ya katibu mkuu huyo haina fikra mpya za kimsingi, lakini inajaribu kusuka pamoja yale ambayo yataweza kukubaliwa na wengi wa wanachama wa umoja huo. Pindi jambo hilo litafanikiwa, basi atakuwa amefanya kazi nzuri kabisa- sawa kabisa ikiwa Ujerumani itakuwa na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ama sivyo.
Huo ndio udondozi wa baadhi ya magazeti ya Ujerumani ya leo.
Miraji Othman