Kikwete, Malala kuendelea kupiga jeki elimu ya Tanzania
18 Julai 2025Wakiwa kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa elimu uliofanyika jijini Dar es Salaam, wawili hao wametahadharisha kwamba mifumo ya elimu barani Afrika iko hatarini kukumbwa na kupunguzwa kwa bajeti kila kunapojitokeza mgogoro wa kimataifa.
Mkutano huo ambao uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete, Mfuko wa Malala na Ushirikiano wa Kimataifa wa Elimu, GPE, umesisitiza kuwa elimu haipaswi kamwe kuwa jambo la pili.
Rais Kikwete alisema elimu ni kiini cha maendeleo yoyote ya kweli na kwamba sio anasa, bali ni njia ya maisha na chombo muhimu cha mabadiliko ya kijamii. Ama alitambua kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kupanua fursa za elimu.
Kuyahusisha majukwaa ya kimataifa
Rais Kikwete na Malala wamekubaliana kuongeza msukumo katika majukwaa ya kimataifa kwa ajili ya kusaka mafungu ya fedha ili kuipiga jeki miradi ya kuendeleza elimu nchini na Afrika kwa ujumla.
Rais Kikwete alisema ushirikiano wao katika miradi ya elimu itawezesha kufadhili shughuli za kuwaendeleza watoto katika kipindi kingine cha miaka mitano kuanzia sasa.
Alisema hali ya dunia kwa sasa inaonesha mwelekeo wa kupunguza fedha za elimu, jambo ambalo ni hatari.
Kwa upande wake, Malala ambaye ni mwanzilishi mwenza wa Mfuko wa Malala na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea alisifu hatua ya kihistoria ya Tanzania ya mwaka 2021 kufuta sera iliyokuwa inawazuia wanafunzi wa kike waliopata mimba kurejea shule.
Alisema uamuzi ule ulikuwa wa kishujaa wa huruma na wa lazima, na ambao ulibadilisha mwelekeo na kutetea haki ya msichana kuendelea na elimu licha ya kuwa mama.
Mabadiliko ya sera yaleta mabadiliko makubwa
Takwimu zinaonyesha kuwa kabla ya sera hiyo kubadilishwa, kati ya wasichana 6,500 hadi 15,000 walifukuzwa shule kila mwaka kwa sababu ya ujauzito, wengi wao wakiwahi kufanyiwa vipimo vya ujauzito kwa kulazimishwa.
Lakini baada ya kubadilishwa kwa sera hiyo wengi wao wanarudi shuleni ndani ya miaka miwili au kuhudhuria vituo mbadala vya kujifunzia.
Hata hivyo, wasichana wengi bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali na kwamba chini ya nusu ya wasichana wa Kitanzania wanahitimu shule ya msingi, na ni asilimia 16 pekee wanaoendelea hadi sekondari ya juu.
Baadhi wanatajwa kukabiliwa na changamoto kama umasikini, mila kandamizi za kijinsia na ukosefu wa miundombinu ya elimu rafiki kwa watoto wa kike.