Kiir amfuta kazi gavana wa jimbo la Upper Nile
20 Machi 2025Katika agizo la rais lililosomwa kwenye runinga ya serikali jana jioni, Rais Kiir alimfuta kazi Oyay kutoka chama cha Machar cha SPLM-IO na kumpa nafasi hiyo James Koang Chuol, luteni jenerali anayetoka Nasir.
SPLM-IO yakasirishwa na hatua ya Kiir
Kufutwa kazi kwa Oyay kulizua hasira kutoka kwa chama hicho cha SPLM-IO ambacho tayari kilikuwa kimejiondoa kwa sehemu katika makubaliano ya amani ya 2018 kufuatia kukamatwa kwa maafisa wake baada ya kundi hilo la White army kuvilazimisha vikosi vya serikali kuondoka katika mji huo wa Nasir ulio karibu na Ethiopia.
Hiki ndicho kitasababisha mvutano mpya Sudan Kusini
Katika taarifa, msemaji wa Machar Puok Both Baluang, amesema kufutwa kazi kwa Oyay ni hatua nyingine ya upande mmoja na ukiukaji mkubwa wa Mkataba huo wa Amani wa mwaka 2018.
Kufutwa kazi kwa Oyay ni hatua ya amani kwa jimbo la Upper Nile
Kwa upande wake, waziri wa habari Michael Makuei, amekishtumu chama cha Machar kwa kuhatarisha makubaliano hayo ya amani na ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hatua ya kumfuta kazi Oyay ni ya kuleta amani katika jimbo hilo la Upper Nile.
Katika hatua nyingine, serikali yaSudan Kusini, jana ilifanya shambulizi lingine la anga dhidi ya raia katika eneo la kaskazini magharibi na kumjeruhi mtoto mmoja. Haya yamearifiwa na afisa mmoja wa eneo hilo pamoja na mashuhuda katika wakati ambapo kuna hofu ya kuzuka upya kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hali inazidi kuwa mbaya mjini Nasir
Kamishna wa kaunti hiyo James Gatluak, amesema shambulizi hilo lilianza alfajiri ya jana wakati jeshi la nchi hiyo lilipoangusha mabomu katika soko la mji wa Nasir kisha baadaye kwenye eneo la makazi.
Uhalifu mpya wa kivita waripotiwa Sudan Kusini
Gatluak amesema hali inazidi kuwa mbaya katika mji huo wa Nasir unaochukuliwa kuwa ngome ya wafuasi wa Machar huku maafisa wa misaada wakiondolewa katika eneo hilo.
Mzozo unazua hofu ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe
Mzozo huo unaozidi kupamba moto, umezua hofu kuwa taifa hilo jipya zaidi ulimwenguni huenda likatumbukia tena kwenye mzozo takriban miaka saba baada ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu.