KIEL : Mtuhumiwa wa ugaidi mbaroni Ujerumani
20 Agosti 2006Nchini Ujerumani polisi imemkamata mtuhumiwa kuhusiana na jaribio la mwezi uliopita la kuripuwa kwa mabomu treni mbili za abiria.
Wamesema mtuhumiwa huyo ambaye ni Mlebanon mwenye umri wa miaka 21 inaaminika kuwa alikuwa ni mmojawapo wa watuhumiwa walionaswa na kamera za uchunguzi katika kituo kikuu cha Cologne hapo tarehe 31 mwezi wa Julai.Hiyo ilikuwa ni siku ambapo yalikutikana mabomu kwenye treni za abiria huko Dortmund na Koblenz pamoja na maneno yalioandikwa kwa Kiarabu.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa katika kituo kikuu cha treni kwenye mji wa bandari ulioko kaskazini wa Kiel.
Wapelelezi wanashuku kwamba mabomu hayo ambayo yalishindwa kuripuka yumkini yakawa yameingizwa ndani ya treni kama sehemu ya njama ya kigaidi.