Khamenei: Mazungumzo na Marekani hayawezi kuzaa matunda
20 Mei 2025Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema kuwa mazungumzo ya nyuklia na Marekani hayawezi kuzaa matunda yoyote, huku kukiwa na mzozo wa kidiplomasia kuhusu shughuli za urutubishaji madini ya urani wa jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Akizungumza Jumanne, Khamenei amesema hadhani kama mazungumzo hayo yatakuwa na matokeo yoyote, na hawajui kitakachotokea.
Kulingana na kiongozi huyo wa kidini, Iran kunyimwa haki ya kurutubisha madini ya urani ni ''kosa kubwa''.
Iran na Marekani zimefanya awamu nne za mazungumzo ya nyuklia tangu Aprili 12, hayo yakiwa mazungumzo yaliyowahusisha maafisa wa ngazi ya juu wa nchi hizo mbili hasimu tangu Marekani ilipojiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya 2015.
Pande hizo mbili zilithibitisha mipango ya kufanya duru nyingine ya mazungumzo wakati wa mkutano wa hivi karibuni wa Mei 11, ambako Iran iliuelezea kama mgumu lakini wenye tija, huku afisa wa Marekani akisema kuwa Washington imetiwa matumaini.