Kesi za kiraia kuendeshwa na mahakama za kijeshi Uganda
16 Juni 2025Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amesaini sheria inayoruhusu mahakama za kijeshi nchini humo kuendesha kesi za kiraia. Hayo yameelezwa na bunge la nchi hiyo leo, katika hatua ambayo viongozi wa upinzani wamesema inakiuka uamuzi uliotolewa na mahakama ya juu.
Wanaharakati wa haki za binadamu kwa muda mrefu wamekuwa wakidai kwamba serikali ya Uganda imekuwa ikitumia mahakama za kijeshi kuwashtaki wapinzani wa kisiasa wa Rais Museveni, ambaye yuko madarakani kwa takriban miaka 40 sasa.
Washirika wake wamekuwa wakikanusha tuhuma hizo wakisema raia wanaoshtakiwa katika mahakama za kijeshi ni wale wanaotumia mtutu wa bunduki kuzusha vurugu za kisiasa.
Mahakama ya Juu nchini humo mwanzoni mwa mwaka huu ilipiga marufuku kitendo hicho ikisema kinakwenda kinyume na katiba.