Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu kusikilizwa mahakama ya wazi
6 Mei 2025Katika kika cha Jumanne, mtuhumiwa Tundu Lissu hakushiriki kwenye kikao hicho kwa njia ya mtandao kama ilivyokuwa ikitarajiwa. Mkuu wa Gereza la Ukonga, Kamishna Msaidizi wa Magereza Juma Mwaibako, aliiambia mahakama kuwa Lissu alikataa kushiriki kwa njia ya mtandao, jambo ambalo linaendana na msimamo wake wa awali kupinga utaratibu huo.
Pamoja na uamuzi wa kuhamishia kesi mahakamani moja kwa moja, Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Yahya aliiomba Mahakama kuahirisha shauri hilo, akieleza kuwa bado uchunguzi haujakamilika.
Soma pia: CCM yaonya hakuna anayeweza kuzuia uchaguzi mkuu
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachowalazimisha kueleza ni hatua gani bado hazijakamilika katika uchunguzi. Alibainisha kuwa mara upelelezi utakapokamilika, taarifa zote zitawekwa katika mfumo wa kielektroniki na kutolewa kwa mawakili wa utetezi.
Kwa upande wao, mawakili wa Lissu wameonesha kutoridhishwa na kauli ya upande wa Jamhuri. Wakili mkuu wa utetezi Rugemeleza Nshala amesema kuna ucheleweshaji usio wa lazima na ameitaka serikali kuharakisha mchakato wa uchunguzi.
Kituo cha sheria chapongeza uamuzi wa mahakama
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Masawe, amepongeza hatua ya kesi kusikilizwa kwa mahakama ya wazi, akisema ni hatua inayoongeza uwazi na haki katika mchakato wa kisheria.
Soma pia: Nyumba za wapinzani Tanzania zazingiriwa na polisi
Kesi hiyo ya uhaini ni miongoni mwa mbili zinazomkabili Tundu Lissu tangu alipofikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Aprili 10, 2025. Kesi nyingine inamhusisha na kuchapisha taarifa za uongo, na zote zinasikilizwa mbele ya Mahakimu wawili tofauti katika Mahakama ya Kisutu.
Hakimu Mfawidhi Franko Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 19, huku akiuagiza upande wa Serikali kukamilisha upelelezi kabla ya tarehe hiyo.