Kesi ya uhaini ya Kabila kuanza kusikilizwa Kinshasa
25 Julai 2025Kabila anakabiliwa na kosa la Uhaini, mauaji na mateso yanayofungamanishwa na kundi la waasi analodaiwa kuliunga mkono la M23.
Makosa mengine anayokabiliwa nayo rais huyo wa zamani ni kushirikiana na vuguvugu la uasi, uhalifu dhidi ya amani na usalama wa binaadamu na kuunyakua kwa nguvu mji wa Goma.
Kabila amekuwa akiitaja serikali ya Felix Tshisekedi kuwa ya kidikteta na amekuwa pia akituhumiwa kushiriki mipango ya kutaka kumuondoa Rais Tshisekedi madarakani.
Joseph Kabila: Rais wa zamani matata alierudi DR Kongo
Hata hivyo rais huyo wa zamani wa Kongo ameitaja kesi yake kuwa ya kizembe na kuituhumu mahakama kutumika kuukandamiza upinzani.
Kabila aliwasili mjini Goma mwezi Mei mwaka huu, wakati mji huo tayari ulikuwa umeshanyakuliwa na waasi wa M23 mwezi Januari. Wiki iliopita serikali ya Kongo ilisaini mkataba wa makubaliano ya usitishaji wa mapigano Mashariki mwa taifa hilo.