Kesi ya uhaini dhidi ya Lissu yasikilizwa Mahakama Kuu
8 Septemba 2025Kesi hiyo hata hivyo imesogezwa mbele hadi Septemba 9, baada ya mvutano mkubwa wa kisheria ulioibuka kuhusu kuahirishwa mara kwa mara kwa kesi hiyo.
Mvutano wa kisheria umeibuka leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam ambako kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu imesikilizwa Jumatatu kwa mara ya kwanza.
Wakati kesi hiyo inaanza, upande wa Jamhuri umesema umemteua mwanasheria kwa ajili ya Lissu ambaye alitambulishwa kwa jina la Neema Saruni, lakini mwenyewe Lissu alikataa kusaidiwa na mwanasheria huyo na badala yake akasema "Nimefanya kazi ya uanasheria kwa miaka 31. Najitetea mwenyewe kwa sababu huu ni mtihani mkubwa. Katika hili, kwa heshima zote nitabeba majukumu yote mwenyewe."
Kesi yasimamishwa kufuatia mvutano wa kisheria
Katika mvutano huo, Lissu alipingana na hoja ya upande wa Jamhuri kuwa kesi yake imeahirishwa kwa mara ya kwanza Agosti 18 mwaka huu na hivyo kutaka apewe nyaraka zinazoonyesha rekodi hiyo kwani kwa rekodi zake, kesi yake imeahirishwa kwa mara ya 10 sasa kabla ya kupelekwa Mahakama Kuu
Mvutano huo wa kisheria ulisababisha mahakama kusimamishwa kwa saa moja, na kurejea tena saa 10 na dakika 10 jioni ya leo.
Baada ya mahakama kurejea, Lissu aliiomba mahakama kumpa muda ili kesho atoe maelezo yake juu ya nyaraka hizo, ambazo anadai zina mashaka, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama na hivyo kesi hiyo itaendelea tena kesho Septemba 9 saa 4 asubuhi
Awali, Lissu aliwasili katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, saa nne kasoro za asubuhi akiwa amezingirwa na walinda usalama, lakini hata kabla ya kuwasili kwake, tayari viwanja vya mahakama hiyo vilikuwa vimeshawekewa ulinzi mkali, wakiwamo polisi wenye mbwa, magari ya polisi na magari ya kusafirisha wagonjwa.
Wadau wa siasa na wawakilishi wa kimataifa wahudhuria
Ilidhaniwa kuwa Lissu angelipanda kizimbani mara tu baada ya kufikishwa lakini hali haikuwa hivyo na badala yake alipanda kizimbani saa sita na nusu mchana, takribani masaa mawili baada ya kuwasili.
Wadau wa masuala ya siasa, viongozi, wanachama wa CHADEMA na wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya waliupamba ukumbi wa mahakama hiyo wakifuatilia kwa umakini kesi hiyo ya uhaini, ambayo imevutia makini za wengi hapa Tanzania.
Kwa upande mwengine, huko mjini Dodoma, kesi ya mgombea urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina na bodi ya wadhamini wa chama hicho dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na mwanasheria mkuu wa serikali iliendelea Jumatatu ambapo walalamikaji wanapinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi kumuondowa Mpina kwenye kinyang'anyiro hicho cha Oktoba 29 mwaka huu.