Kesi ya uhaini dhidi ya Lissu yaahirishwa hadi Juni 2
19 Mei 2025Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefurika wadau wa siasa, wanaharakati wa haki za binadamu, wanasiasa na makada wa Chadema ambao wamekwenda kusikiliza mwenendo wa kesi ya Mwenyekiti huyo wa Chadema, Tundu Lissu.
Miongoni mwa waliofika kusikiliza kesi hiyo ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Kenya David Maraga na Mwanahabari Mkongwe wa Tanzania, Jenerali Ulimwengu. Lissu, akiwa amezingirwa na askari wa usalama aliwasili katika Mahakama hiyo mnamo saa 3 na nusu asubuhi, akiwa ameshikilia begi kubwa lililojaa vitabu.
CHADEMA yapambana na msukosuko mpya wa kisiasa Tanzania
Alipofikishwa ndani ya mahakama akiwa na tabasamu, Lissu alisema hivi, "Hii ya Warioba, Warioba anazungumzia majaji na utendaji wa haki, wanasema nimesema vibaya majaji, warioba ndo msemaji."
Hata hivyo, kesi ya uhaini dhidi ya Lisu ilipotajwa, upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na wanaiomba Mahakama kuahirisha kesi husika kwa siku 14 zaidi, jambo ambalo limepingwa vikali na Mawakili wa utetezi.
Wanaharakati na wanachama wa EALS wazuiwa kuingia Tanzania
Wakati huo huo, wanaharakati na wanachama wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS) akiwamo Mwanasiasa na kiongozi wa chama cha siasa cha Kenya, (PLP) pamoja na aliyewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kenya, Willy Mutunga na wakili wa Chama cha Wanasheria Kenya, Gloria Kimani, wamezuiwa kukanyaga ardhi ya Tanzania na kurudishwa nchini kenya. Karua na wenzake walirudishwa wakiwa Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam ambako walikuja kwa ajili ya kusikiliza kesi ya Lisu.
Akihojiwa na vyombo vya habari baada ya kurudi Kenya, Karua alisimulia kilichowakuta.
"Walitushikilia kwa zaidi ya saa 6, kulikuwa na ofisa aliyetulinda, wakatushikilia kwa saa sita, lakini hawakutufunga pingu," alisema Bi Karua.
Mgombea urais wa zamani wa Kenya, Martha Karua afukuzwa kutoka Tanzania
Uamuzi wa kuwarudisha wananaharakati kutoka Kenya umetafsiriwa kwa mitazamo tofauti na wanasheria nchini Tanzania, ambapo Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) Fulgece Masawe amesema ni muhimu watu kupema nafasi ya kuja kuona kinachoendelea Tanzania.
"Ushauri ni kwamba ni kuwaacha watu washiriki, wanakuja kama wataalamu wa sheria , wanakuja kama watu wa haki za binadamu waachwe washiriki na kuona kinachoendelea," alisema Masawe.
Kesi ya uhaini dhidi ya Lissu imeahirishwa hadi Juni 2 mwaka huu ambapo itasikilizwa kwa njia ya mahakama ya wazi na shauri la uchochezi dhidi ya Lisuu kadhalika bado linaendelea.
Florence Majani, DW Dar es Salaam