Kesi ya Lissu chini ulinzi mkali Dar es Salaam
24 Aprili 2025Lissu anakabiliwa na makosa matatu ya uhaini, uchochezi na kutoa taarifa za uongo. Jeshi la Polisi limeimairisha ulinzi katika viunga vya jiji la Dar es Salaam na katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo wakati kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadena-Taifa Tundu Antipas Lissu ikisikilizwa.
Polisi waliotawanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji na wengi wenye silaha wakiwa katika mahakama ya Kisutu, waliwazuia wanachama wa Chadema na wanahabari kuingia katika viunga vya Mahakama hiyo.
Lissu akataa kesi yake kusikilizwa kwa njia ya mtandao
Wakati hayo yakijiri, taarifa zilizotolewa na makarani wa mahakama zilieleza kuwa kesi hiyo itasikilizwa kwa njia ya mtandao.
Hata hivyo, wakati kesi hiyo ikiendelea kwa njia ya mtandao, askari ambaye jina lake halikupatikana alitoa taarifa kuwa Lisu amekataa kesi yake kusikilizwa kwa njia ya mtandao na badala yake anataka isikilizwe moja kwa moja .
Lisu ambaye katika kesi hiyo anatetewa na jopo la mawakili wakiongozwa na Peter Kibatala amekataa kesi hiyo kusomwa kwa njia ya video kwa madai kuwa sheria iko wazi na anatakiwa kupelekwa mahakamani.
Wakati hayo yakijiri baadhi ya viongozi waandamizi wa Chadema wamekamatwa na polisi na kupelekwa kituoni kisha baadaye kuachiwa. Miongoni mwa waliokamatwa ni John Mnyika, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Heche, Makamu Mwenyekiti-Bara na baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana la chama hicho.
Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu na Mwanasiasa na kiongozi wa chama cha siasa cha PLP cha Kenya, Martha Karua, walifika mahakamani kuonyesha mshikamano katika kesi inayomkabili Lisu.
Soma zaidiChadema yasema Lissu anazuiliwa katika gereza la Ukonga, Dar es Salaam:
Lisu alikamatwa Aprili 9 akiwa wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma akiwa katika mkutano wa hadhara wa kuichechemua ajenda ya chama hicho ya ‘Hakuna mabadiliko; hakuna uchaguzi' na kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam ambako alishtakiwa kwa makosa ya uhaini, uchochezi na kuchapisha taarifa za uongo.
DW: Dar es Salaam