Kenya yawaapisha makamishna wapya wa tume ya uchaguzi
11 Julai 2025Makamishna hao wanajaza nyadhifa muhimu ambazo zilikuwa zimeachwa wazi kwa muda mrefu katika nchi hiyo yenye historia ndefu ya chaguzi zenye utata na mara nyingi zenye vurugu. Mwenyekiti na makamishna sita, ambao watahudumu kwa miaka sita, walikula viapo vyao katika shughuli iliyosimamiwa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Akizungumza kwenye tukio hilo, Koome aliwaambia kuwa wanaingia ofisini katika wakati ambapo taifa linapitia kipindi kigumu, ambapo Wakenya, hasa vijana, wanaonyesha kutoridhika na kusikitishwa na taasisi za umma.
Uchaguzi mkuu ujao wa taifa hilo la Afrika Mashariki utafanyika 2027, lakini tayari Rais Ruto anakabiliwa na shinikizo la maandamano ya mitaani yanayoongozwa na vijana wasioridhika na gharama ya juu ya maisha, ufisadi na ukatili wa polisi.
Jopo la majaji matatu Alhamisi jioni walitupilia mbali ombi lililokuwa limewasilishwa kupinga uteuzi wa Erustus Ethekon Edung kama Mwenyekiti wa Tume hiyo, pamoja na Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol, na Fahima Araphat Abdallah kama Makamishna.
Katika hukumu yao, majaji Roselyne Aburili, John Chigiti na Bahati Mwamuye, walieleza kwamba ombi lililowasilishwa na Kelvin Ray Omondi na Boniface Mwangi halikuwa na msingi wa kisheria na halikuwasilishwa kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha katiba.Hata hivyo, majaji hao walifuta tangazo la gazeti la serikali, lililotolewa na Rais William Ruto la kuwateua makamishna hao, na kuagiza kwamba tangazo jipya la serikali litolewe ili kuhalalishwa uteuzi wao.