Kenya yasimamisha zoezi la kufukua miili huko Binzaro
4 Septemba 2025Daktari wa serikali ya Kenya Richard Njoroge amesema zoezi la kitaalamu la kukusanya vijinasaba kwa miili hiyo litaanza mara baada ya kukamilika kwa vipimo vya mionzi vya X-ray kwenye miili hiyo iliyofukuliwa. Zoezi la hivi karibuni la kufukua miili lilidumu kwa wiki mbili ambapo ilipatikana zaidi ya miili 34 na zaidi ya vipande 100 vya sehemu mbalimbali za mwili.
Mamlaka za usalama zinalihusisha tukio hilo na suala la imani potofu za kidini huku Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja akisema kuwa wataalam kutoka mashirika mbalimbali wanashirikiana ili kubaini chanzo cha vifo hivyo, akiahidi kuwa hivi karibuni watakamilisha uchunguzi.
Washukiwa 11 walikamatwa mwezi uliopita baada ya mwanamke kutoa ripoti kwa polisi kuhusu vifo vya watoto wake. Watu hao watasalia rumande kwa mwezi mmoja zaidi huku polisi wakiendelea na uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo.
Kipi kinaendelea kwa sasa?
Kulingana na nyaraka za mahakama, polisi walikuwa wakifuatilia miamala ya pesa iliyofanyika kwenye simu za washukiwa kutoka kwa watu wanaoshukiwa kufadhili vitendo hivyo. Washukiwa hao walilipia kodi ya nyumba katika mji wa Malindi kabla ya kuhamia kwenye eneo lililojitenga la Chakama katika eneo la Kwa Binzaro kaunti ya Kilifi ambako walijenga vibanda vya udongo karibu na maeneo kulikogundulika miili hiyo.
Mkasa wa mchungaji aliyekuwa akitoa mahubiri hatari Paul Mackenzie unaendelea kuiandama Kenya, ambapo miili kadhaa inaendelea kufukuliwa huko Kilifi ikiwa ni takriban kilomita mbili tu na Shakhahola. Mtaalamu wa masuala ya itikadi kali za kidini Hassan Mwakimako anasema matukio haya ya imani potovu yanahusidhwa na umma kutokuwa na elimu kuhusu dini na kushindwa kwa taasisi.
" Ni kwamba kanuni wakati mwingine si suluhisho kwa matukio kama yale ya Shakahola. Lakini ujuzi, ufahamu, na umakini wa maafisa usalama ni muhimu kuhakikisha kwamba wakati wowote matukio haya yanapotokea, basi hatua za haraka zinachukuliwa dhidi ya wahusika."
Ili kukabiliana na vitendo hivi, serikali ya Kenya iliunda tume ya kuchunguza na kupendekeza sera za kudhibiti harakati za kidini, lakini Mwakimako anasema kuwa udhibiti pekee hautoshi, kwani kinachohitajika ni ufahamu mkubwa wa umma, utoaji wa elimu sahihi ya kidini na hatua za haraka kutoka kwa serikali na vyombo vya usalama.