Kenya yasema marufuku ya Tanzania haitavuruga uhusiano
8 Agosti 2025Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Ujumuishaji wa Kikanda, Mudavadi alieleza kuwa mazungumzo ndiyo njia bora na endelevu zaidi ya kutatua migogoro ya kikanda.
Aidha aliongeza kusema kuwa Kenya haina mzozo wa kidiplomasia na taifa lolote na kwamba serikali imejitolea kuutatua mzozo huu kupitia mazungumzo na kuheshimiana.
Aliwahakikishia wajumbe wa kamati na umma kwa ujumla kuwa serikali imejitolea kikamilifu kushirikiana kwa njia ya kujenga na mataifa jirani ili kulinda amani, kuimarisha ushirikiano, na kuhakikisha uthabiti wa muda mrefu wa eneo hili.
"Kuna masuala tunafaa kusuluhisha, tumesema kuwa masuala hayo yanashughulikiwa na wizara ya masuala ya mambo ya nje, tumewataka masuala hayo yawasilishwe kuhusu biashara, na sera zinazokwenda kinyume cha sera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki", alisema Mudavadi.
"Tunaweza kunufaika licha ya vikwazo vilivyoweka"
Kenya imenufaika pakubwa kutokana na ujumuishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hususan kupitia ongezeko la mauzo ya bidhaa nje na upanuzi wa masoko ya kikanda.
Aidha, Mudavadi alisisitiza kuwa upanuzi wa ujumuishaji wa kikanda ni jambo muhimu kwa kufungua fursa za kiuchumi baina ya nchi. Alieleza umuhimu wa kupunguza vizingiti vya kibiashara na akatoa wito wa kuanzishwa kwa mifumo jumuishi, kama vile miundo ya ujumuishaji mseto, ili kuwasaidia wale ambao bado hawajakamilisha masharti ya ujumuishaji rasmi.
Wakati huo huo Waziri wa Ustawi wa Afrika Mashariki nchini Kenya, Wycliffe Oparanya, akizungumza kwenye maonyesho ya Bisahara ya Afrika Mashariki jijini Nairobi amesema kuwa vikwazo vilivyowekwa na Tanzania vinahujumu biashara miongoni mwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
"Upatikanaji wa soko ni moja ya mambo tutakayoyafanya kuhakikisha kuwa hili soko la Afrika Mashariki la watu milioni 300, tunaweza kunufaika licha ya vikwazo vilivyoweka na baadhi ya wanachama washirika", alisisitiza Oparanya.
Kulingana na taarifa za hivi karibuni, thamani ya biashara ya pande mbili kati ya Kenya na Tanzania kwa sasa inakadiriwa kufikia takribani Dola za Marekani milioni 900 - sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 140 za Kenya au Shilingi trilioni 2.3 za Tanzania kulingana na viwango vya ubadilishaji.