Kenya yapinga sheria mpya za biashara za Tanzania
31 Julai 2025Kupitia taarifa rasmi, Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda ya Kenya imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu amri ya Tanzania iliyoanza kutekelezwa Julai 28, ambayo inawazuia raia wa kigeni kushiriki katika baadhi ya sekta za biashara.
Hatua hiyo imezua mvutano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili. Waziri wa Biashara wa Kenya, Lee Kinyanjui, ameelezea hofu kuhusu sheria mpya ya Fedha ya Tanzania ya 2025 pamoja na marekebisho ya Sheria ya Kodi ya 2019 ambazo zimeongeza kodi ya bidhaa na kodi ya maendeleo ya viwanda kwa asilimia 10 na 15 mtawalia.
Waziri huyo ameihimiza Tanzania kufuta amri hiyo akisema inakiuka misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
"Iwapo kisasi ni moja ya hatua tutakazochukua, ukweli ni kwamba hatuwezi kondoa uwezekano huo, ila ni hatua ya mwisho ambayo huenda tukachukua. Jambo la kwanza ni kutoa nafasi kwa diplomasia na mazungumzo na ndiyo mwelekeo tungependa kuzingatia."
Sheria zinalenga kulinda wafanyabiashara dhidi ya ushindani wa nje
Amri hiyo inakataza raia wa kigeni kushiriki katika nyanja 15 za biashara, zikiwemo saluni, huduma za utalii, miamala ya pesa kwa simu, na urekebishaji wa vifaa vya kielektroniki. Inawahusu wale tu waliokuwa tayari na leseni na inaambatana na adhabu kali kwa watakaokiuka.
Kifungu cha 13 cha mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kinawapa raia wa nchi wanachama haki ya kuanzisha na kuendesha biashara bila ubaguzi katika nchi nyingine mwanachama.
Tamko hilo la Kenya limekuja siku moja baada ya Rais William Ruto kukutana na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambapo walijadili masuala ya kanda na kusaini mikataba minane ya kibiashara.
Rais William Ruto aliwasiliana kwa njia ya simu na Rais Samia Suluhu wa Tanzania kuhusu suala hilo, kama anavyoeleza Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi.
"Mheshimiwa Rais pia kama mwenyekiti wa Kikao cha Jumuiya ya Afrika Mashariki, amewasiliana na Rais wa Jumuiya ya Tanzania na pia Waziri anayehusika na mambo ya Biashara, kwa hivyo tunatumia mbinu za kidiplomasia kutatua yale mumeona kwenye magazeti."
Wakati hayo yakijiri, Kenya na Tanzania zinapanga mikutano ya pande mbili kujadili na kutatua tofauti za kibiashara.
Mkutano wa kiufundi kuhusu biashara ya bidhaa za tumbaku utafanyika Arusha tarehe 4 na 5 Agosti na kikao cha Kamati ya Biashara kimepangwa kufanyika kati ya Agosti 11 hadi 12 kujadili ada na tozo mbalimbali.