Kenya yajiandaa kupambana na ugonjwa usiojulikana
3 Machi 2025Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayehusika na afya ya umma Mary Muthoni anasema tayari maafisa wa serikali kwa ushirikiano na serikali ya jimbo la Kisii tayari wamefika maeneo yaliyoathiriwa kuchukua sampuli za vipimo zitakazofanyiwa uchunguzi chanzo cha maradhi hayo.
Amesema matokeo ya uchunguzi wa maabara yatatolewa kesho Jumanne. Dalili za ugonjwa huo usiojulikana ni pamoja na kuhara damu, kutapika, homa kali na maumivu makali ya kichwa.
Wakaazi walioathiriwa ni wa vijiji vya Nyamarondo, Nyarigiro, Nyabigege vinavyopatikana eneo la Mugirango Kusini.
Vituo vya afya eneo hilo tayari vimeripoti kushindwa kudhibiti idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika kutafuta matibabu ya ugonjwa huo ulioripotiwa kwa mara ya kwanza eneo hilo karibu wiki tatu zilizopita.
Hivi sasa idadi kubwa ya wagonjwa imelazimisha wengi kutumia kitanda kimoja na baadhi yao wamepelekwa jimbo jirani la Migori kwa matibabu.