Kenya yadhibiti uwindaji haramu wa faru kwa miaka mitano
26 Agosti 2025Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Kenya haijaripoti kisa chochote cha uwindaji haramu wa faru. Kulingana na Idara ya Ulinzi wa Wanyamapori nchini Kenya, KWS, matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uangalizi, vikosi vya kupambana na ujangili vilivyopata elimu mwafaka na ushirikiano wa vitengo mbalimbali vya serikali umeleta tija. Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu waKWS, Erastus Kanga, sheria ya usimamizi ya 2013 inayotoa adhabu ya kifungo cha maisha jela au kutozwa faini ya shilingi milioni 20 za Kenya imekuwa silaha muhimu ya kupambana na ujangili.
''Tumeikumbatia teknolojia, kuimarisha uwezo wa vikosi vyetu na kujenga uhusiano mzuri wa kikazi na taasisi nyengine za serikali. Kamwe hatuwapi majangili nafasi ya kujipenyeza.''
Elimu ya umma nayo pia imechangia katika kampeni za kupunguza soko la bidhaa za uwindaji haramu. Miezi miwili iliyopita, Hifadhi ya Lewa ilifanikisha zoezi la kuwafanyia faru mikato kwenye masikio ili kuwawezesha kuwafuatilia kidijitali. Dominic Maringa, Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Lewa, anauisitiziaNdovu na faru huenda wakapungua Tanzaniaumuhimu wa zoezi hilo.
''Tunawafanyia faru mikato masikioni kila baada miaka miwili ili tuweze kuwatambua mmoja mmoja kwenye makundi. Idadi ya faru wanaozaliwa hapa ni kubwa kwa hiyo wanaongezeka kwa wingi kwani mazingira ya mbuga hii yanawapa nafasi nzuri.''
Ifahamike kuwa Kenya ni ya tatu kwenye orodha ya mataifa ya bara la Afrika yaliyo na idadi kubwa ya faru na imepitwa na Afrika Kusini na Namibia pekee. Takwimu za sensa ya mwishoni mwa 2020, zimebaini kuwa kuna jumla ya faru 1,605; ambapo 853 ni weusi na 752 ni weupe. Faru weusi wako katika hali ya hatari kwani idadi yao ilipungua kutokea alfu 20 katika miaka ya 70 hadi chini ya 400 mwaka 1987 kwa sababu ya uwindaji haramu.
Wakati huo huo, ripoti mpya ya Chama cha Wahifadhi wa Mazingira, IUCN na Sekretariat ya Traffic for the Cities imeafiki kuwa uwindaji haramu wa faru barani Afrika umepungua tangu 2021, japo kitisho kijacho ni ukame na mabadiliko ya sera. Ripoti hiyo ilitathimini faru wa Afrika na Asia kwa kuzingatia hali halisi, uhifadhi wao na biashara haramu kabla ya kongamano kuu la mazingira la COP20 lililoratibiwa kufanyika Novemba.
Utafiti huo umeiweka idadi ya faru wa Afrika kuwa 22,540 mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2024. A. Kusini yafanya mnada wa pembe za Faru mtandaoniKwa mujibu wa Grethel Aguilar, Mkurugenzi Mkuu wa IUCN yenye makao yake Uswisi, mafanikio hayo yameletwa na juhudi na elimu ya kisasa ya ufuatiliaji, ushiriki wa jamii na ulinzi ulioimarishwa kwenye mazingira ya wanyamapori.
''Matokeo ya muda mrefu yanahitaji uwekezaji endelevu, nia ya kisiasa na ushirikiano wa kimataifa ili kuwalinda wanyama mbalimbali kwa hali zote.''
Changamoto zinazoiandama Kenya kwa sasa ni kuendelea kupata ufadhili, kuwa na nia ya kisiasa na kuhimili vitisho vinavyoibuka. Endapo hilo litatimia, Kenya itakuwa mfano mzuri na muongozo wa kuhifadhi faru kwa mataifa ambayo yanapambana na uwindaji haramu sugu.