Kenya yaadhimisha miaka 15 ya katiba yake
27 Agosti 2025Kwenye hafla maalum iliyofanyika katika jumba la mikutano la kimataifa la KICC, viongozi wa ngazi ya juu walikusanyika kutathmini hali tangu katiba mpya ya Kenya ya 2010 kuanza kufanya kazi. Rais William Ruto aliitangaza tarehe 27 kuwa siku rasmi ya kutathmini umuhimu wa katiba mpya ya 2010. Akihutubia taifa, Ruto alibainisha kuwa ni wajibu wa kila Mkenya kuilinda katiba.
Itakumbukwa kuwa kiongozi huyo wa taifa aliipinga rasimu ya katiba hiyo wakati wa kampeni za uchaguzi wa awali. Maadhimisho hayo yamezua hisia mseto nje na ndani ya serikali kuu ukizingatia utendakazi na changamoto inazoiandama. Mbunge wa Rarieda Amollo Otiende ambaye ni mwanasheria aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya wataalamu waliohusika na maandalizi ya katiba ya 2010 na anasisitiza kuwa kazi bado ipo.
"Katiba inafanya kazi ila bado changamoto zipo.Tumeweza kuitumia, kutimiza malengo na hata kuwatimua baadhi ya viongozi kwa nguvu hiyo.”
Kenya bado inakabiliwa na jinamizi la ufisadi
Siku ya katiba inaadhimishwa wakati ambapo jinamizi la ufisadi linaisakama serikali ya Ruto ambaye siku chache zilizopita alilituhumu bunge la taifa kwa kuendekeza uovu huo.
Hali hiyo ilimsukuma naibu wa rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua kupuuzilia mbali kauli za serikali na kuinyoshea kidole cha lawama kwa kuitekua katiba ambayo sasa wanaienzi na kuisifia. Gachagua aliyasema hayo saa chache zilizopita ikiwa ni mara ya kwanza kukivunja kimya chake tangu arejee kutokea ziara yake ya Marekani.
Naibu huyo wa rais wa zamani anashikilia kuwa bado anayo nafasi ya kuwani urais katika uchaguzi mkuu ujao mwa mwaka 2027. Ifahamike kuwa kwenye kura ya maoni ya Agosti mwaka 20210, wakenya waliipa ridhaa katiba mpya kwa asilimia 68.6 ya kura.
Chini ya katiba hiyo mpya,mfumo wa serikali za ugatuzi ulizinduliwa, uwajibikaji,utekelezaji na kudumisha haki vyote vilizua hisia za kuwa na mfumo wa uongozi unaowajumuisha wakenya wote.
Katika suala la usawa wa kijinsia uongozini, Kenya bado inasuasua ukizingatia kuwa kufikia sasa asilimia 22 pekee ya wabunge wote 349 ni wanawake hali inayoiweka ya nne kwenye orodha ya idadi ya wabunge wanawake katika mataifa ya Afrika Mashariki.