Kenya: NACADA yasema watoto wadogo wanatumia dawa za kulevya
27 Januari 2021Ripoti hiyo ambayo imewasilishwa bungeni imewalaumu wazazi kwa kuwatelekeza watoto wao wanapowalea. Ripoti Hiyo inaonesha kuwa wanafunzi 500,000 wa shule za sekondari wamewahi kutumia dawa za kulevya. Watoto 370,000 wamewahi kutumia mirungi ama miraa. Ripoti hiyo inaonesha kuwa wanafunzi 314,000 wametumia tumbaku huku 162,000 wakivuta bangi. Wanafunzi 50,000 wamevuta petroli. Inaongeza kusema kuwa wanafunzi 26,058 wanaoenda shuleni wamevuta dawa ya kulevya aina ya Heroine .
Afisa Mtendaji wa NACADA Victor Kioma, anasema kuwa takriban asilimia 7.8 ya watoto katika shule za sekondari wanatumia dawa za kulevya na kwamba hio ni ishara kuwa tunakabiliwa na janga kubwa. Ufichuzi huo unajiri huku serikali ikishinikiza mabadiliko kwenye sheria ya kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya. Serikali inapania kuongeza adhabu kali kwa wakosaji kwa kuwatoza shilingi milioni 50 pamoja na kuwafunga.'
Wengine wanaolengwa na muswada huo
Muswada huo ambao umewasilishwa na NACADA pia unawalenga maafisa wa polisi wanaoshirikiana na walanguzi, ili kukwepa sheria. Mishi Mboko mbunge wa Likoni anasema vita hivyo ni vigumu kuvikabili, kwani kuna baadhi ya maafisa wa polisi wanaohusika.
Kinachosikitisha zaidi ni kuwa, dawa hizo za kulevya zinachangia kwa utovu wa nidhamu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Ripoti hiyo inasema kuwa idadi ya wanafunzi wanaotumia mihadarati huenda ikawa ya juu zaidi kwa sababu visa vingi haviripotiwi. Inasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa watoto ambao wazazi wao wanatumia dawa za kulevya, kuzitumia pia.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wazazi wanastahili kuwajibika na kuzingatia tabia za watoto wao badala ya kuwaachia walimu majukumu ya ulezi. Ripoti hiyo inakamilika kwa kusema kuwa, mazingira ya shule za msingi na sekondari sio salama kwani dawa za kulevya zinatumika na wanafunzi.