Kenya na China katika mkakati wa maendeleo endelevu
24 Aprili 2025Marais hao wameazimia kuimarisha ushirikiano wa siku zote kwa kusisitiza umoja na mshikamano miongoni mwa mataifa yanayoendelea hasa wakati huu dunia ikikabiliwa na misukosuko.
Kupitia kauli ya pamoja baada ya kikao chao mjini Beijing katika ziara anayoifanya nchini China Rais wa Kenya William Ruto viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa kupitia nia ya pamoja kati ya China na Afrika.
Kulindwa na kutetea maslahi ya mataifa yanayoendelea
Wameahidi kulinda na kutetea maslahi ya nchi zinazoendelea na kuhamasisha sera za utandawazi jumuishi hususan wakati huu wa mizozo ya kisiasa ulimwenguni.
Rais Xi Jinping wa China ameonya nia yake ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili kama hatua ya kukabiliana na misukosuko ya kisiasa na kiuchumi ulimwenguni huku akisisitiza kuwepo kwa mahitaji ya kuimarisha zaidi mfumo imara wa ushirikiano miongoni mwa mataifa ya ulimwengu.
Kauli ya viongozi hawa wa Kenya na Chinainakwenda sambamba na mkakati mkubwa wa kuweka ushirikiano imara na endelevu barani Afrika kupitia mkakati mpana wa China wa ujenzi wa miundo-mbinu ya barabara na usafirishaji maarufu kama Belt and Road Initiative au BRI kwa ufupi.
Kenya ni mdau muhimu wa mradi Belt and Road Initiative au BRI
Kenya ni mdau muhimu katika mkakati huu kutokana na kwamba China imefadhili miradi mikubwa nchini Kenya kama vile ujenzi wa Reli kati Mombasa-Nairobi na kwa sasa Kenya imetangaza kuhitaji ufadhili zaidid kutoka China katika ujenzi zaidi wa reli hiyo hadi nchini Uganda kwenye muktadha mpana wa kurahisisha usafiri na usafirishaji katika kanda nzima. Rais William Ruto amepongeza ushirikiano kati ya Kenya na China.
Rais Ruto amenukuliwa akisema "Natazamia kuimarisha zaidi ushirikiano wetu ambao umekuwepo, kujenga uelewa zaidi kati ya watu wetu wa pande mbili na kuhakikisha kwamba tunapeleka azimio hili mbele zaidi, Kenya ni mdau wa mkakati huu wa BRI wa ujenzi wa miundombinu ya barabara na kwa mantiki hiyo tuna reli yenye umbali wa kilomita 600 kuanzia Mombasa-Nairobi hadi Naivasha. Tuna bandari ya Lamu tuna eneo maalum la kushushia mafuta katika bandari ya Mombasa, barabara za mwendo kasi Nairobi na miradi mingine ya ujenzi wa barabara. Haya yote ni ushahidi wa ushirikiano baina ya nchi zetu mbili.” Alisema kiongozi huyo wa Kenya.
Kenya na China zatia saini mikataba 20 ya ushirikiano
Katika ziara hii ya Rais William Ruto nchini China marais hawa pia wametia saini mikataba 20 ya ushirikiano katika Nyanja za sayansi na teknolojia,elimu, miradi ya maji,biashara za mitandaoni, usafirishaji kwa kutumia akili-mnemba na maendeleo ya miundombinu kwa ujumla. Pia suala ushirikiano katika sekta za afya na ulinzi hasa kupeana taarifa za kuhusu ughaidi wa kimataifa na pia kuweka na mfumo wa pamoja katika mazoezi ya kijeshi limekubaliwa
Licha ya changamoto za kiuchumi ikiwa ni pamoja kiwango kikubwa cha madeni, Rais Rutoamehakikisha utayari wa Kenya kufikia malengo yake ya kiuchumi na kifedha. Aliposhika hatamu za uongozi mwaka 2022 aliahidi kupunguza matumizi, kuinua kiwango cha kukusanya mapato na kuepuka kushindwa kulipa madeni ya nje.
Ziara ya Ruto nchini China inabadili sera ya kigeni kwa Kenya, wakati akionekana mwanzo kuwa mdau mkubwa wa nchi za magharibi na Marekani, sintofahamu inayoendelea kwa sasa baina ya Marekani na China inaifanya Kenya kufikiria upya katika sera hii ya katika mataifa ya kigeni.
Jitihada ya kupinga sera za vikwazo za mataifa ya magharibi
Kwa upande wake Rais Xi wa China anasema anathamini ushirikiano wake na Kenya huku akiutaja kama wa kutolea mfano katika nchi zinazoendelea. Nchi mbili zimetangaza kupinga sera za vikwazo vya nchi za magharibi kwa kuweka vipingamizi katika biashara huria na pingamizi katika teknolojia huku viongozi hao wakiahidi kushirikiano kupinga zaidi sera hizo za magharibi kuhusu uchumi na biashara.
Soma zaidi:China na Kenya zatangaza kuimarisha zaidi mahusiano
Pande mbili pia zinatathmini suala la usafiri wa anga baina ya Nairobi na Beijing huku China ikitazamia kufuangua ubalozi mdogo kati mji wa Guangzhou ambao ni maarufu katika biashara na viwanda.