Kenya, Morocco zatinga robo fainali michuano ya CHAN
18 Agosti 2025Imesonga mbele baada ya kuitandika Angola bao 1-0 katika mchezo wa kukata na shoka ulipigwa Jumapili jioni mjini Nairobi.
Wenyeji hao wenza wa michuano hiyo iliyoandaliwa kwa pamoja pia na Tanzania na Uganda, walipata ushindi huo kupitia goli lililowekwa wavuni mnamo dakika ya 75 na mshambuliaji machachari Ryan Ogam.
Ushindi huo uliiwezesha Kenya kuongoza kundi A na kufanikiwa kutinga robo fainali. Timu nyingine ya kundi hilo, Morocco, nayo imefuzu kucheza robo fainali kutokana na ushindi wa bao 3-1 iloupata kwenye mchezo wake dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Tanzania na Madagascar tayari zilikwishajikatia tiketi ya kucheza robo fainali. Mechi za lala salama kwa hatua ya makundi zitaendelea leo Jumatatu na kesho Jumanne kutafuta timu nyingine nne zitakazosonga mbele.