Kenya kuuza chai nje na kuwatenga mawakala
23 Mei 2025Kabla ya vita kuanza, Chad isiyokuwa na bandari ilipokea bidhaa zake kupitia Sudan. Kwa sasa Chad inatazamwa kama mteja wa moja kwa moja wa chai ya Kenya japo inapokea bidhaa inazoagizia kutoka nje kupitia mataifa jirani ya Nigeria na Cameroon. Mary Muthoni, mkaazi wa Abogeta West, Meru anaisifia biashara hiyo.
”Biashara ya chai iko sawa na thabiti, mamlaka ya majani chai ya KTDA ndio inayosaka soko la zao letu. Kazi yetu ni kupanda na kuvuna kisha wao wanakamilisha safari.” alisema Mary. Doreen Karendi naye ni mkaazi wa Tharaka Nithi na analalamikia hatua hiyo.
"Sasa najiuliza, nikichuna majani hiyo bei itakuwaje? Soko likiharibika hatujui tutaendawapi.Tofauti ni kuwa vile walivyokuwa wakinunua hilo halipo tena.”anafafanua Karendi.
Mkataba wa ushirikiano kati ya Kenya na Umoja wa Ulaya kuanza hivi karibuni
Ili kuipa msukumo hoja ya kusaka wateja wapya, hivi karibuni, Rais William Ruto alikutana na wawekezaji kutoka mkoa wa Fujian, China pamoja na ujumbe wa wadau wa sekta ya chai nchini kujadili mbinu za kukiongeza kiwango cha bidhaa hiyo inayouzwa China. Kwa sasa Kenya inaiuzia China kilo milioni 12.42 za chai na inanuwia kuziongeza hadi kilo milioni 50 ifikapo mwaka 2030. Willie Kimutai ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Chai nchini Kenya na anasisitiza kuwa mustakabali wa chai unaleta matumaini.
"Kuna soko jipya tumefungua la China.Tunatarajia kuwa kiwango cha chai kinachovunwa sasa hivi kitaongezeka bei hadi mara tatu ya iliyoko sasa tukiuza chai yenye ubora wa juu.”
Pakistan ndiye mteja mkubwa wa chai ya Kenya
Kwa mujibu wa Bodi ya Chai nchini Kenya, bei ya kilo ya chai mnadani imeshuka kutokea dola 2.68 za Kimarekani hadi dola 2.25 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ili kupambana na hilo, mwishoni mwa mwaka uliopita, Kenya ilifutilia mbali kigezo cha bei ya chini ya akiba ya dola 2.34 kwa kilo katika mnada wa Mombasa ili kuchagiza mahitaji na kuongeza ushindani ili kupunguza mrundiko uliofikia kilo milioni 100. Pakistan ndiye mteja mkubwa wa chai ya Kenya ambayo hununua kiasi ya theluthi moja ya zao lote linalouzwa nje. Mamlaka ya Chai nchini Kenya iko mbioni kusaka wateja wapya, na pia kulinda maslahi ya wakulima. Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Chai katika kiwanda cha chai cha Gitugi kaunti ya Nyeri, Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe alisisitiza kuwa mwelekeo mpya ni kuondoa mawakala katika biashara ya chai kwa manufaa ya mkulima.
Kwa upande wake, Shirika la Wafanyabiashara wa Chai katika eneo la Afrika Mashariki, EATTA, linairai serikali kukaa kwenye meza ya mazungumzo na Sudan ili kuwapa wateja muda wa kununua majani ya chai ambayo tayari yalishaondoka mikononi mwa wakulima yaliyoko safarini au kwenye mabohari mjini Mombasa. Sudan iliiwekea Kenya marufuku ya kuuza majani ya chai ndani ya mipaka yake baada ya kuwapokea waasi wa RSF ambao wamekuwa wakipambana na serikali kuu kwa miaka miwili sasa.
Thelma Mwadzaya, DW Meru-Kenya.