Kenya kuziondoa sheria zote zilizopitwa na wakati
3 Februari 2025Kenya ina idadi kubwa ya sheria zilizopitwa na wakati, hasa kwenye masuala kama vile urithi, ndoa, mahusiano ya kifamilia, na haki ya jinai. Sheria hizi kwa kiasi kikubwa ni mabaki ya utawala wa kikoloni wa Uingereza ambayo iliitawala Kenya mpaka mwaka 1963.
Aidha, kitengo cha mahakama kuu kinachoshughulikia masuala ya kikatiba kimetangaza kuwa baadhi ya vipengele vya sheria za bunge vinakinzana na katiba. Mwanasheria Mkuu wa Kenya Dorcas Oduor amesema ofisi yake imeanza mchakato wa kuzirekebisha sheria hizo au kuziondoa kabisa.
"Tunataka kutumia tume ya marekebisho ya sheria kuchukua uongozi katika kuzitambua sheria hizi na kuzishughulikia. hivi karibuni tutakuwa na mkutano wa kushughulikia sheria zote ambazo ni kinyume cha katiba au zilizopitwa na wakati ili tuangalie ikiwa zinafaa kwa madhumuni.” Alisema Oduor.
Soma pia:Umoja wa Mataifa yasema "sheria kandamizi" zinatumika mkoa wa Xinjiang
Kenya ina sheria nzima iliyotungwa mwaka wa 1925, kuhusu uchawi ikilenga kudhibiti vitendo vya kishirikina na madhara yake katika jamii.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio ambapo watu wametuhumiwa kwa uchawi na kuchukuliwa hatua za kisheria au hata kuuawa na wanajamii wenye hasira.
Kwenye baadhi ya matukio katika maeneo ya pwani na magharibi nchini Kenya watu wanaotuhumiwa kuwa wachawi waliuawa kwa sababu ya migogoro ya ardhi, ambapo neno "uchawi" linatumiwa kuhalalisha mauaji hayo.
Sheria za kudhibiti makanisa
Sheria za kudhibiti makanisa pia zimekuwa na mianya. Mnamo Juni 2023, jopo kazi lililoteuliwa na Rais William Ruto lilianza kupitia sheria zinazodhibiti makanisa nchini Kenya. Hii ilitokana na matukio ambapo baadhi ya viongozi wa kidini walitumia mianya katika sheria hizo kufanya vitendo vya kihalifu.
Idadi ya watu waliofariki baada ya mchungaji Mkenya kuamuru wafuasi wake wafe kwa njaa ili kukutana na Yesu ilizidi watu 300. Hii ilionyesha kuwa sheria zilizopohazikuwa zimejumuisha mabadiliko ya kijamii na kiutamaduni, hivyo kuhitaji marekebisho ili kukabiliana na changamoto za sasa.
Wanasheria na watetezi wa haki za binadamu wanasema nyingi ya sheria hizo hazizingatii mahitaji ya sasa ya kijamii ya Kenya na nyingi ya sheria hizo zinachukuliwa kuwa za kibaguzi na ambazo zinahitaji mageuzi makubwa.
Wakili Shadrack Mose amesema ushirikiano na mashirika mengine ya serikali ni muhimu kuhakikisha agenda zinazotekelezwa nchini zinaambatana na sheria zilizoko kwenye katiba ya Kenya.
"Na tunawaambia washirika wetu kwamba wanaweza kujiinua, kuungana, kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha kuwa wana huduma muhimu katika kaunti hizo.”
Soma pia:UN: Maelfu ya waandishi habari wakimbia nchi zao kutokana na ukandamizimakenzipaul
Pamoja na hayo, Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor amesema ujio wa serikali za kaunti pia umeleta matukio ya kujirudia kwa sheria.
"Baadhi ya matukio ambapo tuna sheria zinazokinzana ni pale tunapogundua kuwa serikali za kaunti zinakuja na sheria katika mada sawa ambapo serikali ya kitaifa tayari ina sheria. Kwa mifano katika udhibiti wa pombe, leseni na zaidi.”
Shughuli hiyo inaendelea sambamba na zoezi la kutoa hamasa kwa umma ili kurahisisha sheria na kuifanya ieleweke kwa watu, hatua ambayo itazisaidia jamii zisizojiweza kufikia haki.
Vilevile wanatafuta njia ambapo wanaweza kutumia teknolojia kuziba pengo la umaskini kwa kumuwezesha kila mtu kuelewa mchakato wa sheria.