Je, Kenya inahatarisha uhusiano wake wa kipekee na Marekani?
6 Agosti 2025Uamuzi wa Marekani kuipa Kenya hadhi ya mshirika mkuu asiye mwanachama wa NATO (MNNA) mwezi Mei 2024 ulionekana kama ushindi mkubwa wa kidiplomasia kwa Rais William Ruto.
Hadhi hiyo, ambayo ni ya kipekee barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ilifungua mlango wa usaidizi wa kijeshi, kijasusi na kiusalama kati ya Kenya na Marekani, pamoja na kuiweka Nairobi kama miongoni mwa wachezaji muhimu wa Marekani katika eneo la Afrika Mashariki.
Hata hivyo, hali imeanza kubadilika. Ripoti kutoka kwa vyombo vya habari vya Kenya zinaonyesha kuwa Bunge la Marekani limeanzisha mchakato wa kutathmini upya hadhi hiyo, kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni "mwelekeo wa kutia shaka” wa sera za kigeni za Kenya.
Maseneta kama James Risch wameelezea wasiwasi wao kuhusu kile walichokiita "mgeuko wa kushangaza wa Kenya kuelekea China na Iran,” ambao huenda ukaathiri usalama wa eneo lote na kuharibu ushirikiano wa kimkakati uliokuwepo kati ya Nairobi na Washington.
Siasa ya kupiga teke kila meza: Kenya kati ya Mashariki na Magharibi
Katika ziara yake ya kitaifa mjini Beijing mwezi Aprili 2024, Rais Ruto alinukuliwa akisema kuwa "mfumo wa sasa wa dunia umevunjika na hauwezi tena kufanikisha maendeleo ya kweli." Aliendelea kueleza dhamira ya Kenya na China kuwa "wabunifu wa mpangilio mpya wa dunia.”
Kauli hiyo, iliyoambatana na ushawishi mkubwa wa China nchini Kenya kupitia mikopo na miradi ya miundombinu, ilionekana na baadhi ya wachambuzi kama ishara ya kuhamia kwenye ushawishi wa Mashariki.
Mambo haya hayaishii kwa China pekee. Rais Ruto pia alielezea Iran kama "mshirika wa kimkakati wa Kenya” wakati wa ziara ya aliyekuwa Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, jijini Nairobi mwaka 2023. Hii imeongeza hofu kwa Marekani, ikizingatiwa kuwa Iran ni adui mkubwa wa Washington na inahusishwa na harakati mbalimbali zenye misimamo mikali Mashariki ya Kati.
Lakini je, Kenya inajaribu kusawazisha nguvu za dunia kwa manufaa yake ya kiuchumi na kieneo, au imeanza kupoteza mwelekeo wa kidiplomasia?
Serikali ya Marekani pia inataka kufahamu kama msaada wa kijeshi na kijasusi iliyoipa Kenya umetumika vizuri, hasa ikizingatiwa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa maandamano ya kihistoria mwezi Juni 2024.
Hali ilivyo sasa inaonyesha kuwa Kenya imefika njia panda ya kihistoria. Iwapo itakosa kueleweka vizuri katika hatua zake mpya za kidiplomasia, huenda ikapoteza nafasi yake ya kipekee na ya kimkakati katika macho ya Marekani.
Katika dunia inayozidi kugawanyika kati ya Mashariki na Magharibi, Kenya inalazimika kujiuliza: Je, inaweza kupiga teke kila meza bila hatari ya kupoteza kiti chake kabisa?