Israel kujenga "taifa la Kiyahudi la Israel"
30 Mei 2025Katz ameyasema haya siku moja baada ya serikali ya Israel kutangaza kubuniwa kwa makaazi mengine 22 mapya katika mamlaka hiyo ya Palestina.
"Hili ni jawabu kwa makundi ya kigaidi yanayojaribu kudhoofisha hatua yetu ya kulidhibiti eneo hili, na pia ni ujumbe wa wazi kwa Macron na marafiki zake. Watalitambua taifa la Palestina kwenye karatasi tu ila sisi tutalijenga taifa la Kiyahudi la Israeli kwenye ardhi," alisema Katz.
Makaazi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi ambayo yanachukuliwa kama kigingi kikuu katika kupatikana kwa amani ya kudumu, hukosolewa pakubwa na Umoja wa Mataifa kama yaliyo kinyume cha sheria za kimataifa.
Hayo yanafanyika wakati ambapo mashambulizi ya anga ya Israel yamesababisha vifo vya watu 14 katika Ukanda wa Gaza. Haya yamesemwa na maafisa wa hospitali katika ukanda huo.
Mashambulizi hayo yametokea wakati ambapo wanamgambo wa Hamas wanalipitia pendekezo la usitishwaji mapigano la Marekani lililoidhinishwa na Israel.
Mjumbe wa Marekani huko Mashariki ya Kati wiki hii alikuwa ameelezea matumaini ya makubaliano ya kusitishwa mapigano na misaada zaidi ya kiutu kukubaliwa kuingia Gaza.