Karua ashangazwa na hatua dhidi ya Lissu
25 Aprili 2025Martha Karua alionekana kortini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ambapo kesi ya Tundu Lisu, ilipangwa kusikilizwa na baadaye kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Wakili huyo, ambaye pia amewahi kuwa Waziri kwa nyakati tofauti katika serikali ya Kenya, amesema amekuja Tanzania kama mwanasiasa, kama mwanasheria nak ama mwana jumuiya ya Afrika Mashariki huku akisisitiza serikali ya CCM ifungue mazungumzo kati yake na Chadema.
"Hatuaacha haki za wana Afrika Mashariki kudhulumiwa, nchi zizingatie mfumo wa kisheria na haki za binadamu. Tanzania kuna uchaguzi Oktoba, serikali ya CCM inataka kumtaabisha Tundu Lisu, ili kuwaondoa wapinzani na wavuke bila kupingwa", alisema Karua.
Akiwa mahakamani hapo, Karua aliambatana na mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki, mwakilishi wa shirika la Amnesty na wanasiasa kutoka Kenya lakini walikumbana na kadhia ya polisi kupiga watu hivyo baadhi ya wawakilishi hao wakaondoka mahakamani.
"Jeshi la polisi lililazimika kuwakamata"
Kesi hiyo ya uhaini na uchochezi inayomkabili Tundu Lisu ilifanyika kwa njia ya mtandao huku kukiwa na vuta nikuvute kati ya polisi na baadhi ya wafuasi na viongozi wa Chadema.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jeshi la polisi lililazimika kuwakamata na kuwahoji, baadhi ya viongozi wa Chadema ili kulinda usalama. Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro
"Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam lililazimika kuwakamata na Kwenda kuwahoji, baadhi ya watuhumiwa katika matishio ya suala la usalama katika mahakama ile, wakiwamo watu wafuatao, John Mnyika, John Heche, na Chacha Heche Seguta", alisisitiza Muliro.
Wakili wa Chadema, Dk Lugemeleza Nshala akiliwakilisha jopo la mawakili wanaomtetea Lissu amesema mteja wao hayaogopi mashtaka yanayomkabili na hivyo anataka shauri lake liwe wazi ili aweze kujitetea hadharani.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini aliahirisha kesi hizo mbili ambapo kesi ya uhaini dhidi ya Lisu itasikilizwa Mei 6 na kesi ya uchochezi itasikilizwa Aprili 28 zote kwa njia ya mtandao.