KARLSRUHE: Mahakama ya Ujerumani yaamuru raia wa Ujerumani anayetuhumiwa kwa ugaidi aachiliwe huru
18 Julai 2005Mahakama kuu nchini Ujerumani imeamuru kuachiliwa huru kwa mtuhumiwa wa kundi la al-Qaeda. Mahakama ya sheria mjini Karlsruhe ilizingatia malalamiko ya raia wa Ujerumani mwenye asili ya Syria, Mamoun Darkazanli, kwamba kumpeleka nchini Uhispania kujibu mashtaka yanayomkabili ni kinyume cha sheria msingi za Ujerumani.
Mahakama imesema waranti iliyotumiwa kumkamata Darkazanli mwaka jana mjini Hamburg haitoi maelezo ya kutosha ya kuwalinda raia wa Ujerumani kisheria. Maofisa wa Uhispani wanamtaka bwana huyo ayajibu mashtaka ya ugaidi.
Waranti za umoja wa Ulaya zinazolenga kuboresha ushirikiano katika kuwakamata na kuwashtaki watuhumiwa wa kigaidi, zitakuwa halali wakati sheria mpya zitakapoanza kufanya kazi. Sheria hizo zitawaruhusu majaji kuifanyia marekebisho amri ya kuwarejesha wajerumani kujibu mashtaka katika mataifa walikofanya makosa.