Karibu waandamanaji 10 wauawa Nepal
8 Septemba 2025Tovuti kadhaa za mitandao ya kijamii - ikiwa ni pamoja na Facebook, YouTube na X imefungwa nchini Nepal tangu Ijumaa baada ya serikali kuzuia majukwaa 26 ambayo hayajasajiliwa, hatua iliyosababisha hasira kubwa ya umma.
"Hadi sasa waandamanaji 10 wamekufa na 87 wamejeruhiwa," Shekhar Khanal, msemaji wa polisi wa bonde la Kathmandu, aliiambia AFP.
"Umati bado uko mitaani"
Wengi wa waliojeruhiwa walikuwa wakitibiwa katika hospitali moja ya kiraia iliyo karibu na waliko waandamanaji.
Kwa mujibu wa afisa wa habari wa hospitali hiyo, Ranjana Nepal, hajawahi kuona hali ya kutatanisha kama inayoshuhudiwa sasa hospitalini hapo.
"Mabomu ya machozi yaliingia hadi kwenye eneo la hospitali na kufanya mazingira ya kazi kwa madaktari kuwa magumu," aliongeza.
Wakiwa wanapeperusha bendera za taifa, vijana hao waandamanaji katika mji mkuu, Kathmandu, walianza maandamano kwa wimbo wa taifa kabla ya kuimba nyimbo za kupinga marufuku ya mitandao ya kijamii na ufisadi.
Umati ulifurika karibu na jengo la bunge na ghasia zilizuka mitaani huku polisi wakipambana na waandamanaji ambao baadhi yao waliparamia ukuta ndani ya majengo hayo ya bunge.
Maandamano kama hayo yalifanyika pia katika maeneo mengine kote nchini humo.
Majukwaa maarufu ya mitandaoni, kama vile Instagram, yana mamilioni ya watumiaji nchini Nepal ambao wanayategemea kwa burudani, habari na biashara.
'Tunataka mabadiliko'
Mmoja ya waandamanaji na mwanafunzi Yujan Rajbhandari, mwenye umri wa miaka 24, alisema: "Tulichochewa na marufuku ya mitandao ya kijamii lakini hiyo sio sababu pekee ya sisi kukusanyika hapa," aliongeza "Tunapinga ufisadi ambao umekomaa hapa Nepal."
Tangu kupigwa marufuku, video zinazotofautisha mapambano ya Wanepali wa kawaida na watoto wa wanasiasa wanaojivunia anasa na likizo za gharama kubwa zimeenea kwenye TikTok, mtandao ambao bado unafanya kazi.
"Kumekuwa na vuguvugu nje ya nchi dhidi ya ufisadi na serikali inahofia hilo linaweza kutokea hapa pia," mwandamanaji Bhumika Bharati alisema.
Baraza la mawaziri liliamua mwezi uliopita kuzipa kampuni zilizoathirika siku saba za kujiandikisha nchini Nepal kuwa na anuani ya kuwasiliana na kuteua afisa wa kushughulikia malalamiko na wa ufuatiliaji.
Uamuzi unafuatia amri ya Mahakama ya Juu mnamo Septemba, 2024. Katika taarifa ya siku ya Jumapili, serikali ilisema inaheshimu uhuru wa mawazo na kujieleza na imejitolea "kuunda mazingira ya ulinzi na matumizi yao bila vikwazo".
Serikali ya Nepal mnamo mwezi Julai iliuzuia mtandao wa ujumbe wa Telegram ikisema unachangia ongezeko la ulaghai mtandaoni na utakatishaji fedha. Mwezi Agosti mwaka uliopita, iliondoa marufuku ya miezi tisa kwa mtandao wa TikTok baada ya jukwaa hilo kukubali kufuata kanuni za nchi hiyo.