Karibu 20% ya dawa za kansa Afrika ni duni au bandia
1 Julai 2025Takwimu mpya zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu huenda wanatumia dawa ambazo hazina viambato muhimu vinavyohitajika kuzuia au kupunguza kasi ya saratani. Hayo ni kulingana na utafiti uliochapishwa wiki hii na jarida la The Lancet Global Health, uliochunguza sampuli kutoka hospitali 12 na maduka ya dawa 25 katika nchi za Ethiopia, Kenya, Malawi na Cameroon.
Watafiti walijaribu karibu aina 200 za dawa za saratani kutoka kampuni tofauti. Matokeo yalionyesha kuwa karibu asilimia 17 ya dawa hizo, sawa na moja kati ya dawa sita, zilikuwa na viwango visivyo sahihi vya viambato hai, hata zile zilizotumika katika hospitali kubwa.
Dawa zenye viambato visivyotosha zinaweza kushindwa kudhibiti uvimbe wa saratani, na hata kusababisha usambaaji wake zaidi mwilini. Ingawa visa vya dawa duni za antibiotiki, malaria na kifua kikuu vimeripotiwa awali, huu ndio utafiti wa kwanza kufichua kiwango kikubwa cha dawa bandia za saratani barani Afrika.
Lutz Heide, mtaalamu wa famasia kutoka Chuo Kikuu cha Tübingen nchini Ujerumani, alisema hakushangazwa na matokeo hayo. Ingawa hakuhusika moja kwa moja katika utafiti huo, alisifu ripoti hiyo kwa kutoa mwanga juu ya suala hilo.
Sababu ni nyingi, lakini haziko wazi moja kwa moja
Sababu za tatizo hili ni nyingi na si rahisi kuzikabili moja kwa moja. Kwa mujibu wa Marya Lieberman wa Chuo Kikuu cha Notre Dame nchini Marekani, alieongoza utafiti huo - sababu zinaweza kuwa kasoro katika utengenezaji, hali mbaya za hifadhi, au uwepo wa bidhaa bandia kabisa. Dawa bandia huongeza uwezekano wa tofauti kubwa kati ya kilicho kwenye lebo na dawa halisi.
Kutambua dawa duni au bandia ni changamoto kubwa. Mara nyingi, wataalamu wa afya au wagonjwa hulazimika kutegemea uchunguzi wa macho — kama vile kuangalia rangi au maandiko ya dawa. Lakini katika utafiti huu, ni chini ya robo moja ya dawa duni zilizogundulika kwa njia hiyo. Zilizosalia zilibainika kupitia uchunguzi wa maabara.
Lieberman anasema suluhisho ni kuimarisha usimamizi na kutoa teknolojia na mafunzo kwa maabara za nchi husika, na kuongeza kuwa bila uwezo wa kupima huwezi kuzisimamia. Dawa za saratani ni sumu kali na ni ngumu kuzichambua, ndiyo maana maabara nyingi hazitaki kushughulika nazo. Lieberman aliongeza kuwa maabara nyingi katika nchi za Afrika hazina vifaa salama vya kushughulikia dawa za kemikali kali kama hizo.
Tatizo halihusishi dawa za saratani pekee
Karibu muongo mmoja uliopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) liligundua kuwa moja kati ya dawa kumi zinazotumika katika nchi za kipato cha chini na cha kati ni bandia au duni.
Utafiti mwingine umeonyesha kuwa viwango hivyo vinaweza kuwa mara mbili zaidi. Mbali na madhara ya kiafya kama kushindwa kwa matibabu au athari mbaya za dawa, kuna pia hasara za kiuchumi kwa jamii na serikali zinazotumia fedha nyingi kununua dawa zisizo na ufanisi.wa dawa unafuatiliwa kwa karibu na taasisi za udhibiti zina uwezo mkubwa wa kubaini na kuondoa dawa za mashaka. Lakini katika nchi nyingi za Afrika, miundombinu ya kudhibiti, vifaa vya maabara, na usimamizi wa soko la dawa ni hafifu. Wagonjwa hulazimika kununua dawa katika masoko yasiyo rasmi kutokana na gharama ya juu ya dawa zilizosajiliwa.
WHO imesema inashirikiana na mamlaka za kitaifa katika nchi nne zilizohusika kwenye utafiti ili kukabiliana na tatizo hilo. Shirika hilo pia limesisitiza wito wake wa muda mrefu kwa nchi kuimarisha mifumo ya udhibiti wa dawa ili kuzuia visa vya dawa za viwango duni au bandia, hasa katika programu za saratani.